Libya yaomba boti, helikopta kukabili wahamiaji haramu
26 Aprili 2017Serikali ya Ujerumani inasema orodha ya maombi hayo kwa ajili ya kikosi cha Libya cha ulinzi wa pwani pia inajumuisha , magari ya kubebea wagonjwa, vifaa vya mawasiliano na vile vinavyoweza kutumika kuona nyakati za usiku.
Kwa mujibu wa jibu la serikali ya Ujerumani kupitia swali lililoulizwa bungeni kutoka kwa mbunge wa chama cha Die Linke, halmashauri ya Umoja wa Ulaya inatafakari kuhusu ombi hilo.
Kituo cha televisheni ya taifa cha ARD nchini Ujerumani kimeripoti leo kwamba Libya inataka baadhi ya maboti hayo yawe na silaha.
Umoja wa Ulaya unataka kuzuwia wahamiaji kuvuka bahari na kuingia katika bara la Ulaya kutoka nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, ambayo imetumbukia katika machafuko tangu mwaka 2011 baada ya kuangushwa kutoka madarakani kiongozi wa muda mrefu, Moammar Gaddafi.