1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya inatafakari kuitisha usaidizi wa kimataifa

15 Julai 2014

Serikali ya Libya imesema inatafakari kuomba msaada wa vikosi vya kigeni kuweza kukabiliana na hali ya usalama nchini humo baada ya makabiliano makali kusababisha kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Tripoli

https://p.dw.com/p/1Cd0J
Picha: Reuters

Mapigano kati ya makundi hasimu ya wanamgambo wanaong'ang'ania udhibiti wa madaraka umesababisha kufungwa kwa uwanja wa kimataifa wa Tripoli na kulifanya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika kuendelea kuhisi kutengwa.

Hapo jana umoja wa Mataifa ulitangaza unawaondoa wafanyakazi wake wote waliokuwa wamesalia nchini humo kwa sababu ya kudorora kwa hali ya usalama.

Maafisa wa Libya wamesema kulizuka upya mashambulizi jana jioni katika uwanja huo wa ndege ambao umefungwa ambapo maroketi kadhaa yalirushwa, mojawapo likigonga ndege moja na kumuua askari na kuwajeruhi wengine sita. Asilimia tisini ya ndege zilizokuwa zimeegeshwa katika uwanja huo zimeharibiwa na maroketi hayo.

Libya kuomba msaada kudhibiti usalama

Muda mfupi baada ya mashambulizi hayo ya jana, serikali kupitia msemaji wa waziri mkuu Ahmed Lamin imesema inatafakari uwezekano wa kuomba msaada wa vikosi vya kijeshi vya kigeni kuisadia kurejesha usalama na kuisaidia kuwa na nguvu za kutekeleza mamlaka yake.

Waziri mkuu wa Libya Ahmed Maiteeq
Waziri mkuu wa Libya Ahmed MaiteeqPicha: Reuters

Jumuiya ya kimataifa iliingilia kati nchini Libya na kusaidia kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011,matokeo yake sasa yakiwa Libya kutokuwa na uthabiti kufuatia mivutano na malumbano kati ya makundi hasimu ya wanamgambo waliomng'oa madarakani Gaddafi na kuliyumbisha taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

Mapigano yamezidi tangu uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita na kusababisha Umoja wa Mataifa kuwoandoa wafanyakazi wake.Taarifa kutoka umoja huo imesema kuwa uamuzi huo wa kuwaondoa wafanyakazi wake wote jana ni wa muda tu na kwamba watarejea punde hali ya usalama itakapoimarika na kuruhusu mazingira mazuri ya kufanya kazi na kuishi.

Makundi ya hasimu ya wanamgambo yaiyumbisha Libya

Uwanja huo wa ndege wa Tripoli ulifungwa Jumapili baada ya wanamgambo wa kundi la Zintan kushambuliwa na kundi jingine la wanamgambo. Hapo jana Libya pia ilisitisha shughuli zote za usafiri za kuingia na kutoka katika uwanja wa ndege wa Misrata ambao unategemea uwanja wa Tripoli kuendesha shughuli zake.

Majengo yaliyo Karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli
Majengo yaliyo Karibu na uwanja wa ndege wa TripoliPicha: picture-alliance/AP Photo

Tangu kung'olewa madarakani na baadaye kuuawa Gaddafi,Libya imeshuhudia machafuko ya karibu kila siku na serikali za muda ambazo zimeingia madarakani tangu wakati huo zimekuwa na kibarua kigumu kurejesha hali ya kawaida kutokana na misukosuko,kushindwa kuyadhibiti makundi ya wanamgambo na tofauti za kisiasa.

Nchi jirani na Libya Algeria, Chad, Misri, Sudan na Tunisia hapo jana zilitaka kuwepo kwa mdahalo na kukubaliana kuunda tume mbili zitazosimamia mazungumzo na kujaribu kuzuia kusambaa kwa ghasia hizo za Libya.

Umoja wa Ulaya umelitaka bunge jipya la Libya lililochaguliwa mwezi uliopita kukutana haraka iwezekanavyo na kuunda serikali mpya inayoungwa mkono na wengi kisiasa itakayoweza kuzuia kuendelea kwa ghasia.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel