1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leyen aonya kuhusu janga la corona

2 Oktoba 2020

Rais wa halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen akionya kwamba janga la COVID 19 barani Ulaya kwa mara nyingine linatia wasiwasi na bado kunasalia umuhimu wa kuwa wangalifu zaidi katika kukabiliana nalo. 

https://p.dw.com/p/3jLnC
Belgien Brüssel | Pressekonferenz Brexit | Ursula von der Leyen
Picha: Johanna Geron/AP Photo/picture-alliance

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekutana kwa siku ya pili hii leo mjini Brussels kujadili masuala kadhaa, wakati rais wa halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen akionya kwamba janga la COVID 19 barani Ulaya kwa mara nyingine linatia wasiwasi na bado kunasalia umuhimu wa kuwa wangalifu zaidi katika kukabiliana nalo. 

Wakuu hao wamekutana kwenye makao makuu ya Umoja huo kujadiliana masuala yanayohusiana na soko la pamoja, sera za viwanda na mabadiliko ya kidijitali, baada ya hapo jana kukubaliana kuiwekea vikwazo Belarus na mapema leo kukubaliana kuwawekea vikwazo kiasi watu 40 nchini humo baada ya Cyprus kuondoa upinzani wake dhidi ya masharti kwamba umoja huo pia utaiadhibu Uturuki kufuatia hali ya wasiwasi mashariki mwa bahari ya Mediterrania.

Von der Leyen amenukuliwa akisema hali ya maambukizi ya COVID 19  ni ya kutia wasiwasi, hivyo wanatakiwa kuwa waangalifu zaidi ili kuzuia kurejea hali mbaya iliyoshuhudiwa katika majira ya mwaka huu ya machipuko. Von der Leyen alikuwa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano na wakuu hao mjini Brussels.

Hata hivyo, von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya umepiga hatua katika mchakato wa kupata chanjo muhimu dhidi ya virusi hivyo vipya vya corona na kuongeza kuwa ni suala la msingi katika upatikanaji wa suluhu ya muda mrefu dhidi ya mzozo huo.

UK Brexit Verhandlungen | Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson anakabiliwa na shinikizo kufuatia nia yake ya kukikuka makubaliano ya BrexitPicha: AFP/N. Halle'n

Mbali na janga la corona, von der Leyen ametoa wito kwa mazungumzo ya biashara kuimrishwa baada ya kumalizika kwa raundi ya mwisho iliyopangwa ya mazungumzo kuhusiana na mustakabali wa mashirikiano kati ya Ulaya na Uingereza.

"Kwa hivyo utaona kutokana na maneno yangu, bado kuna kazi kubwa ya kufanya, lakini ni kama ninavyosema, ni suala la haki. Na ikiwa unataka kulifikia kikamilifu soko moja, kanuni za usawa lazima zitumike, kwa hivyo hii ni ngumu sana, lakini pamoja na yote penye nia pana njia. Kwa hivyo nadhani tunapaswa kuimarisha mazungumzo kwa sababu inafaa kuyafanyia kazi kwa bidii." alisema.

Aidha waziri mkuu wa Ireland Micheal Martin ameitaka Uingereza kuhesimi makubaliano kuhusiana na suala tete la mpaka wa Ireland wakati mazungumzo ya wiki hii kati ya Umoja huo na London yakishindwa kuziba pengo lililopo katika makubaliano ya kibiashara.

Soma Zaidi: Mpango wa Uingereza wa Brexit waibua wasiwasi Umoja wa Ulaya

Katika hatua nyingine kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema makubaliano yoyote kati ya China na Umoja wa Ulaya kuhusu uwekezaji yanatakiwa kuwa ya manufaa kwa pande zote, kwa makampuni ya Ulaya kuwa na uhuru sawa wa kuwekeza China, kama china inavyofanya Ulaya. Amesema, vikwazo dhidi ya makampuni ya Ulaya yanayotaka kuwekeza China bado vilikuwa juu mno.

Aidha Merkel amesema wakuu hao wameujadili mzozo unaopamba moto kati ya Arzebaijan na vikosi vya kikabila vya Armenia katika jimbo la Nagorno-Karabakh, wakiangazia usitishwaji mapigano hayo haraka iwezekanavyo na kusema ndio njia pekee kuelekea mazungumzo ya amani kuhusu suluhu ya mzozo mgumu kati yao.  

Mashirika: RTRE