1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lesotho yataka kuwa na ushawishi mkubwa katika michezo ya barafuni

Josephat Charo13 Agosti 2007

Lesotho inataka kuwa nchi maarufu barani Afrika katika michezo ya kuteleza kwenye barafu. Nchi hiyo yenye ukubwa kama wa Ubelgiji barani Ulaya inataka kuwa eneo muhimu la michezo ya barafuni barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHbJ
Mashindano ya marathon kwenye barafu
Mashindano ya marathon kwenye barafuPicha: AP

Ollie Esplin, meneja wa kampuni ya Afri-Ski amesema Lesotho itakuwa na eneo kubwa la kufanyia michezo ya kuteleza kwenye barafu katika bara zima la Afrika. Meneja huyo ameeleza vipi hatari ya kuyeyuka barafu katika bonde la Mahlasela inavyotarajiwa kuendelea kupungua katika siku za usoni. Waafrika Kusini wanaokwenda nchini Lesotho kufanya likizo zao tayari huteleza kutumia njia ya pekee iliyopo katika bonde la Mahlasela.

Katika miaka ijayo njia nyengine nne zitajengwa na kuwekewa vizuizi vitakavyoweza kupitika kwa urahisi na vingine vitakavyotoa changamoto kubwa kwa wachezaji. Vijumba takriban 100 vinatarajiwa kujengwa pamoja na uwanja wa mchezo wa Golf utakaokuwa juu zaidi duniani ukijengwa katika kima cha mita 3,300 kutoka kima cha bahari.

Vibanda kadhaa tayari vimejengwa katika maeneo ya milima nchini Lesotho. Licha ya vibanda hivyo kusafirishwa kutoka nchini Estonia, bado kuna uasili wa kiafrika katika eneo hilo. Kutoka mikokoteni inayosukumwa na ng´ombe na nyumba za kitamaduni zilizojengwa kutokana na udongo uliochanganywa na kinyesi cha ng´ombe, yote haya yanayafanya mazingira kuwa ya kupendeza na barabara nyembamba zinazoelekea kwenye eneo la michezo ya kuteleza barafuni.

Cha kufurahisha zaidi ni kwamba eneo hilo liko mwisho wa dunia, na wala sio kama maeneo ya michezo hii barani Ulaya, amesema meneja Esplin.

Tangu miaka ya 1970, wachezaji wa michezo ya barafuni wamekuwa wakisafiri kwenda nchini Lesotho, ingawa meneja Esplin anasema hajui idadi yao. Mwaka jana watu 5,000 katika eneo kunakofanywa michezo ya barafuni aidha walikodisha vifaa vya kufanyia michezo au kuvinunua. Angalau mara moja kwa mwaka watu huenda katika eneo hilo.

Ili kuzuia barafu kuyeyuka kwa haraka, waanzilishi wa kampuni ya Afri-Ski kutoka Austria na Afrika Kusini wamechukua hatua za tahadhari. Meneja wa kampuni hiyo, Ollie Esplin, amesema mtu anapojenga njia ya kuteleza kwenye barafu, hususan barani Afrika, sharti ielekee kusini ambako itapata joto kidogo la jua.

Meneja huyo ameisifu Lesotho akiitaja kuwa Uswissi ya eneo la Kusini, ingawa nchi hiyo ni miongi mwa mataifa maskini barani Afrika. Raia wengi wa nchi hiyo wanaishi katika umaskini uliokithiri huku wakitegemea sana kilimo.

Kozi moja ya mafunzo ya kuteleza barafuni inayodumu muda wa saa nne hugharimu kiwango cha euro 42, kiwango ambacho ni wachache sana wanaoweza kukimudu. Mshahara wa wastani kwa kila Mlesotho unakadiriwa kuwa chini ya euro 750 kila mwaka. Ni watalii pekee, hasa kutoka mkoa wa Gauteng nchini Afrika Kusini, wanaoweza kugharamia michezo ya kuteleza barafuni katika maisha yao.

Katika michezo ya kuteleza barafuni Lesotho haina upinzani kwenye bara la joto kama Afrika. Ni eneo la Tifendell pekee nchini Afrika Kusini ambako mtu anaweza kuteleza katika barafu. Kwa sasa kunapatikana njia tatu za kutelezea katika eneo hilo na kozi ya mafunzo ya michezo ya kuteleza barafuni hugharimu euro 120.

Kwa wachezaji kutoka miji mikubwa ya Johannesburg na Pretoria, kampuni ya Afri-Ski mbali na bei ndogo ya kozi zake, inavutia wengi kwa sababu nyengine. Billy Becker, raia wa Afrika Kusini anasema hahitaji kusafiri mwendo mrefu kwani ni safari ya saa nne tu kufika eneo hilo linalomjaza mhemuko.

Lebohang Ramonotse ni miongoni mwa watu wanaojifunza kuteleza katika barafu. Kwa kawaida yeye huuza katika eneo la bonde la Mahlasela. Anatumai eneo hilo la michezo ya barafuni litatengeza nafasi za ajira kwa wakaazi. Anasema mpango walio nao ni mkubwa ingawa anajua sio Walesotho wengi walio na mawazo kama yake.

Lakini hata meneja wa kampuni ya Afri-Ski anaamini matokeo yatapatikana. Kuna mpango wa kujenga mahala pa kufanyia mafunzo ya hali ya juu na kufanyia pia mazoezi.