1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lesotho yamzika mkuu wake wa majeshi aliyeuawa

15 Septemba 2017

Mfalme wa Lesotho, Letsie wa Tatu, amesema mauaji ya kamanda wa jeshi la nchi hiyo wiki iliyopita yameleta ''aibu'' na ''hofu'' kwenye nchi hiyo ndogo ya kifalme.

https://p.dw.com/p/2k2qa
Lesotho - Armeechef Khoantle Motsomotso
Picha: Flickr/US Army Africa/Medical Readiness Excercise 14-1

Khoantle Motsomotso aliuawa kwa kupigwa risasi na wapinzani wake wa kijeshi kwenye nchi hiyo ambayo inaendelea kukumbwa na mzozo wa kisiasa na kijeshi.

Mfalme Letsie, ambaye ni nadra sana kutoa hotuba za umma, alikuwa akiwahutubia waombolezaji katika maziko ya kamanda huyo aliyevamiwa wiki iliyopita katika kambi ya jeshi.

Maziko ya kamanda huyo yamefanyika katika kijiji kilichoko umbali wa kilomita 80 kaskazini mwa Maseru na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji.

Mfalme ambaye anaheshimika katika nyanja zote za kisiasa, amewasihi viongozi kuacha kulitumia jeshi katika michezo michafu ya kisiasa.

Pia amelitaka jeshi kumuunga mkono kamanda mpya wa jeshi, Meja Jenerali Lineo Poopa, kufanya kazi kwa bidii ili kuliondoa jeshi katika matatizo hayo makubwa