Lesotho: Chama cha Waziri Mkuu chamtaka ajiuzulu
10 Januari 2020Chama tawala nchini Lesotho kimemtaka waziri mkuu wa nchi hiyo Thomas Thabane ajiuzulu kuhusiana na madai ya kuhusika na kifo cha mkewe mwaka 2017, kikimuita kuwa ni kitisho kwa taifa.
Katika nyaraka za mahakama zilizopatikana wiki hii, mkuu wa polisi nchini humo amemshutumu Thabane kwa kuhusika katika kifo cha Lipolelo Thabane nje kidogo ya mji mkuu Maseru siku mbili kabla ya mume wake kuapishwa.
Shutuma hizo zinakuja baada ya waziri mkuu kusimamisha kazi kamishna wa polisi Holomo Molibeli ambaye uchunguzi aliouendesha umefichua kuwa namba ya simu ya mkononi ya Thabane ilikuwa katika rekodi za mawasiliano ya siku yalipofanyika mauaji hayo.
Thabane ambaye ana umri wa miaka 80, alikuwa katika mchakato wenye mvutano mkubwa na mkewe wa kutaka talaka.