1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni leo msema kesho ni muongo Obama na Clinton wakabana koo

Josephat Charo3 Machi 2008

Uchaguzi wa awali kumtafuta mgombea urais wa Marekani kufanyika katika majimbo ya Texas na Ohio

https://p.dw.com/p/DHWQ
Seneta wa jimbo la Illinois Obama (kushoto) na seneta wa jimbo la New York ClintonPicha: AP

Seneta Barack Obama ameongeza juhudi zake za kuyazika matumaini ya seneta Hillay Clinton kutaka kuteuliwa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, huku uchaguzi wa awali ukitarajiwa kufanyika leo katika majimbo ya Texas na Ohio.

Seneta Hillary Rodham Clinton anang´ang´ania kuokoa juhudi zake za kuwania uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic baada ya kushindwa mara 11 mfululizo na mpinzani wake seneta Barack Obama.

Katika uchaguzi wa awali utakaofanyika Jumanne wiki hii katika majimbo makubwa ya Texas na Ohio, seneta Clinton ana matumaini ya kumshinda Obama na kuendelea kubakia katika kinyang´anyiro na pengine hatimaye kuweza kushindana na mgombea wa chama cha Republican John McCain katika kuwania urais wa Marekani.

Seneta Obama wa jimbo la Illinois ana nafasi nzuri ya kumshinda Clinton katika majimbo yote mawili ya Texas na Ohio ingawa matokeo ya kura ya maoni yanaonyesha akiongoza kwa pointi chini ya asilimia nne. Obama anaongoza kwa asilimia 47 katika jimbo la Texas dhidi ya Clinton mwenye asilimia 44. Hata hivyo seneta Clinton amejiongezea pointi moja kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na shirika la Zogby International.

Mgombea wa chama cha Republican, John McCain, anaonekana atapata ushindi mkubwa katika majimbo ya Texas na Ohio. Anaongoza kwa idadi kubwa ya wajumbe dhidi ya mpinzani wake mkubwa, gavana wa zamani wa jimbo la Arkansas, Mike Huckabee. McCain, seneta wa jimbo la Arizona, anakaribia kushinda uteuzi wa chama cha Republican na anaongoza kwa idadi kubwa ya wajumbe watakaomteua mgombea wa chama kuwania urais wa Marekani, ambayo wagombea wengine hawataweza kuifikia.

Miungano ya wapigaji kura kutegemewa

Wagombea wote wa chama cha Democratic bado wanategemea miungano ya wapigaji kura katika jimbo la Texas na Ohio, iliyowasaidia kushinda katika mashindano ya awali, huku Clinton akipat akura za wanawake, wazee, wafuasi wa chama cha Democratic wa tangu jadi na wamarekani wenye nasaba ya kihispania. Obama kwa upande wake anawavutia wapigaji kura wanaume, vijana, wamarekani weusi na watu binafsi wasioegemea upande wa Republican au Democratic.

John Zogby wa shirika la Zogby Internationala anasema atakayeshinda Texas Mashariki atakuwa na nafasi ya kushinda katika jimbo hilo.

Clinton anaongoza kwa idadi ndogo ya kura katika jimbo la Ohio, ishara kwamba mfululizo wa ushindi wa Obama huenda ukakatizwa. Asilimia 6 ya wafuasi wa chama cha Democratic jimboni Texas bado hawajaamua wanataka kumpigia kura nani.

Kwa upande wa chama cha Republican, John McCain anaongoza kwa asilimia 61 kwa 28 katika jimbo la Ohio na kwa asilimia 53 kwa 33 katika jimbo la Texas dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Mike Huckabee.

Obama ajitetea

Barack Obama amejiepusha na mashambulio ya Clinton kuhusu uwezo wake katika sera ya kigeni. Mzozo mpya kuhusu usalama wa kitaifa ulizuka huku wafuasi kadhaa wa Obama wakiongeza shinikizo dhidi ya Clinton kumtaka amuachie Obama uteuzi wa urais wa chama cha Democratic iwapo atashindwa kupata ushindi mkubwa katika majimbo ya Texas na Ohio.

Clinton alisema Jumamosi iliyopita kwamba kampeni yote ya Obama inazungumzia hotuba ya kupinga vita ya mwaka wa 2002. Obama ambaye huenda akawa mmrekani wa kwanza mweusi kuwa rais wa Marekani, amesema wakati wa kupitisha uamuzi kuhusu sera muhimu ya kigeni katika kizazi hiki, uamuzi wa kuivamia Irak, seneta Clinton alifanya makosa.

Obama amesema mpaka leo Clinton hajakiri alifanya makosa kuunga mkono vita dhidi ya Irak au kusema uamuzi wa kuivamia nchi hiyo ulikuwa kosa.

Bill Clinton awatolea mwito wapigaji kura

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, amewatolea mwito wapigaji kura wampigie kura mke wake Hillary kwa kuwa ndiye mgombea pekee atakayeiacha Marekani katika mahala pazuri wakati awamu yake ya urais itakapomalizika.

Bill alitoa mwito huo wakati wa mkutano wa hadhara katika bustani la Houston juzi Jumapili mbele ya umati wa watu 1,200 wafuasi wa mke wake Hillary. Clinton pamoja na mtoto wake wa kike, Chelsea, walihudhuria ibada ya asubuhi katika kanisa la Lakewood mjini Houston, ambalo lina idadi kubwa ya waumini nchini Marekani.