Leo ni kufa na kupona kwa Uhispania
18 Juni 2014Kocha wa Australia Ange Postecoglou anaamini kuwa kikosi chake kinalazimika kushambulia iwapo kinataka kuwa kikosi kilichozusha mshangao katika kombe la dunia leo, wakati itakapopambana na Uholanzi ambayo inaogelea katika furaha ya kuwakandika mabingwa watetezi Uhispania mabao 5-1.
Vijana hao maarufu kwa jina la "Soccerroos" wanahitaji kupata kitu kutoka katika mchezo huo iwapo watataka kuvuka na kuingia katika timu 16 bora zitakazohimili vishindo vya awamu ya mtoano, licha ya kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Chile katika mchezo wa kwanza.
Postecoglou anaamini kuwa kushambulia ndio njia sahihi ya kujilinsa katika mchezo huo wakati wanatafakari jinsi ya kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Uholanzi Robin Van Persie na Arjen Robben , ambao wote walipachika mabao mawili kila mmoja katika mchezo wao dhidi ya Uhispania.
Mabingwa watetezi Uhispania wamepata kipigo cha kudhalilisha cha mabao 5-1 dhidi ya Uholanzi katika mchezo wao wa kundi B, na mabingwa hao wa kombe la dunia mwaka 2010 na mabingwa mara mbili wa kombe la mataifa ya Ulaya , watakuwa hawana chao iwapo watashindwa kupata ushindi dhidi ya Chile .
Ni mabingwa watetezi watatu ndio walishindwa kuvuka kikwazo cha kwanza, Brazil mwaka 1966, Ufaransa mwaka 2002, na Italia mwaka 2010, na mchezaji wa kati wa Uhispania Andres Iniesta anafahamu kuwa Uhispania inakabiliwa na changamoto kubwa kuweza kunusurika.
"Chile ni timu ngumu kwasababu tutahitaji kulinda lango letu vizuri na tutalazimika kupambana mchezaji kwa mchezaji," amesema mchezaji huyo wa kati wa Barcelona , mfungaji wa bao lililowapa ubingwa wa dunia Uhispania mwaka 2010 nchini Afrika kusini.
Wiki moja baada ya kuanza fainali hizi za kombe la dunia Croatia inataka kuweka alama yake katika michuano hii. Croatia inaingia katika mpambano wa leo(18.06.2014) wa kundi A dhidi ya Simba wa Nyika Cameroon wakitambua kuwa kipigo walichopata katika mchezo wa ufunguzi ni lazima wakiweke kando. Cameroon pia inajikuta katika hali kama hiyo.
"Tunafahamu nini maana ya hali hii, kwetu na kwa Cameroon," kocha wa Croatia Niko Kovac amesema jana. Kila mmoja anaweza kufanya hesabu. Si lazima kuingia katika mazungumzo hayo.
Lakini kimsingi mchezo wetu wa pili na wa tatu ni muhimu mno, kwasababu hawa ni washindani wetu kwa nafasi ya pili," Kovac amesema .
Iwapo timu yoyote kati ya hizo itashinda michezo yake miwili iliyobaki, itajihakikishia nafasi katika duru ijayo ya mtoano.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape afpe
Mhariri:Yusuf Saumu