1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leipzig, Freiburg, Hamburg nusu fainali kombe la shirikisho

Josephat Charo
3 Machi 2022

RB Leipzig ilipata ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Hanover katika mechi ya robo fainali ya kuwania kombe la shirikisho la Ujerumani Jumatano (02.03.2022) kudhihirisha wao ndio wanaopigiwa upatu wa kushinda kombe hatimaye.

https://p.dw.com/p/47x4d
DFB-Pokal | Viertelfinale | Hannover 96 - RB Leipzig | Tor (0:2)
Christopher Nkunku, kulia, akitia kimyani bao la pili dhidi ya HanoverPicha: Matthias Koch/imago images

Christopher Nkunku alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza na Konrad Laimer na Andre Silva wakaongeza mabao kwa Leipzig, klabu ambayo imewahi kukamilisha msimu wa Bundesliga katika nafasi ya pili mara mbili katika historia yao.

Timu nyingine ya Bundesliga yenye fursa ya kushinda kombe la shirikisho ni Freiburg ambao walifanikiwa kuingia nusu fainali ya kombe la shirikisho kwa kuilaza Bochum 2-1.

Klabu inayocheza ligi ya daraja la pili HSV Hambrg ilikosa mkwaju wa penalti lakini ikajitahidi kutoka nyuma kwa mabao mawili na kulazimisha sare 2-2 dhidi ya Karlsruhe ambayo ilicheza na wachezaji 10. Baadaye Hamburg ilishinda pambano la robo fainali 3-2 kupitia mikwaju ya penalti ambapo mlindalngo Daniel Heuer Fernandes aliokoa mikwaju miwili ya penalti

Union Berlin iliichapa St Pauli Hamburg 2-1 siku ya Jumanne kujikatia tiketi ya nusu fainali ambayo droo yake itafanyika Jumapili na mechi kuchezwa Aprili 19 na 20. Fainali imepangwa kuchezwa Mei 21 katika uwanja wa Olympic Stadium mjini Berlin.

Mabingwa wa zamani wa mashindano ya Ulaya, Hamburg, ambao walishinda mikwaju ya penalti kwa mara ya tatu mfululizo, ndio timu pekee ya ligi ya daraja la pili na klabu pekee iliyowahi kushinda kombe la shirikisho, iliyo miongoni mwa timu zilizofanikiwa kuingia nusu fainali, ushindi wa mwisho wakiupata mnamo 1987.

RB Leipzig ilianzishwa miaka 22 baadaye, mwishoni mwa mwaka 2009, na kufadhiliwa na kampuni ya kutengeneza vinywaji ya Red Bull, ikapoteza fainali ya mwaka uliopita dhidi ya Borussia Dortmund na 2019 dhidi ya Bayern Munich. Lakini huku miamba wote wawili wa soka la Ujerumani wakiwa wameshabanduliwa kwenye mashindano haya, Leipzig sasa wanawekewa matumaini makubwa kama timu bora na walidhihirisha hilo katika mechi ya Jumatano walipoitwanga Hanover.

Kiungo wa Leipzig, Kevin Kampl, alisema, "Tulidhibiti mchezo kikamilifu na tulistahiki kuingia nusu fainali. Tunataka kuandika historia."

(dpa)