Lebanon yatafuta usaidizi wa kidiplomasia kuhusu Waziri Mkuu
9 Novemba 2017Lebanon inaamini kuwa Saad al-Hariri aliyejiuzulu kama waziri mkuu Jumamosi iliyopita akiwa saudi Arabia anashikiliwa Saudi Arabia na serikali ya nchi yake inapanga kushirikiana na wanadiplomasia wa kigeni ili kumrudisha nyumbani. Wakati huohuo, al-Hariri amekutana na balozi wa Ufaransa nchini Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa afisa mmoja mkuu wa serikali ya Lebanon, Saad al-Hariri anashikiliwa na Saudi Arabia na sasa juhudi zinafanywa kwa ushirikiano na wanadiplomasia kuwezesha kurudishwa kwake nyumbani.
Katika chanzo cha pili cha habari, mwanasiasa mmoja mkuu ambaye ana uhusiano wa karibu na Saudi Arabia amesema Saudi Arabia ilimumuru al-Hariri kujiuzulu kisha kumweka katika kifungo cha nyumbani.
Katika duru ya tatu ya habari, afisa mmoja anayefahamu hali ilivyo amesema Saudi Arabia inamdhibiti na kuzuia safari zake.
Al-Hariri alishawishiwa kuziuzulu?
Kujiuzulu kwa al-Hariri ambako kulitangazwa moja kwa moja kwenye kituo cha televisheni akiwa saudi Arabia, kumeitumbukiza Lebanon katika mzozo wa kisiasa na mgogoro katika kanda hiyo kati ya Saudi Arabia na Iran.
Hatua hiyo imezusha minong'ono kuwa mwanasiasa huyo wa madhehebu ya Sunni na rafiki wa muda mrefu wa Saudi Arabia, ameshawishiwa kujiuzulu na Wasaudi Arabia.
Saudi Arabia na wanachama wa vuguvugu la Hariri la Future Movement wamezikanusha ripoti kuwa al-Hariri ameshikiliwa kwenye kizuizi cha nyumbani. Mwenyewe hajatoa taarifa inayopinga madai kuwa safari zake zimezuiliwa au zimedhibitiwa.
Al-Hariri akutana na wanadiplomasia
Kupitia taarifa yake, afisi ya Hariri imesema kuwa amekutana na balozi wa Ufaransa nchini Saudi Arabia leo Alhamisi, na kwamba jana Jumatano alikutana na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Saudi Arabia na siku ya Jumanne alikutana na balozi wa Uingereza na mkuu wa masuala ya Marekani nchini Saudi Arabia.
Saudi Arabia imesema Hezbollah ambayo ilijumuishwa katika serikali ya muungano ya Hariri, imeuteka mfumo wa kisiasa wa Lebanon.
Hezbollah kwa upande wake imeitaka Saudi Arabia kutoingilia masuala ya Lebanon ikisema hatua ya Hariri kujiuzulu akiwa Riyadh inaibua maswali mengi.
Katika hotuba yake ya kujiuzulu, Hariri alizishambulia Iran na Hezbollah kwa kupandikiza chuki miongoni mwa nchi za Kiarabu na akasema alihofia angeuawa. Baba yake ambaye alikuwa waziri mkuu mkongwe wa zamani aliuawa kwa bomu mnamo mwaka 2005.
Rais Aoun amtaka Hariri kurudi nyumbani kueleza sababu za kujiuzulu
Afisa mmoja mkuu serikalini Lebanon aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa kwa sababu serikali haijaweka wazi msimamo wake, amesema Lebanon inaelekea kuziomba nchi za kigeni na za kiarabu kuiwekea Saudia Arabia shinikizo ili imuachilie Saad al-Hariri.
Afisa huyo ameongeza kuwa Hariri angali Waziri Mkuu wa Lebanon, kauli inayoshikiliwa na maafisa wengine wanaosema kuwa Rais Michel Aoun hajapokea rasmi barua ya Hariri ya kujiuzulu.
Aoun anataka arudi Lebanon na aeleze sababu zake za kujiuzulu kabla achukua uamuzi.
Mwandishi: John Juma/RTRE/APE
Mhariri: Mohammed Khelef