Lebanon yaomboleza mauaji ya wafuasi saba wa upinzani
28 Januari 2008Waziri mkuu wa Lebanon, Fouad Siniora, ameamuru shule zote pamoja na vyuo vikuu vifungwe hii leo huku nchi hiyo ikiomboleza vifo vya wafuasi saba wa upinzani waliouwawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano yaliyofanywa jana mjini Beirut.
Waandamanaji waliokasirishwa na mgao wa umeme walikabiliana na wanajeshi wa Lebanon katika mapambano mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha mwaka mmoja.
Mamia ya waislamu wa madhehebu ya shia wanaoipinga serikali ya Lebanon, waliandamana na kuchoma matairi kufunga barabara kuu za mjini Beirut na vitongoji vya kusini.
Katika taarifa yake waziri mkuu Fouad Siniora ameyalaani vikali mauaji ya waandanaji hao yaliyofanywa katika vitongoji vya kusini mwa Beirut na kuwataka Walebanon wawe watulivu na wasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanywa na jeshi na maafisa wa usalama.