1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon-mapigano yamemalizika ?

22 Juni 2007

Kinyume na ilivyotangazwa jana,yaonesha mapigano bado hayajamalizika kabisa nchini Lebanon kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa kiislamu katika kambi ya wapalestina ya Naher el Bared.

https://p.dw.com/p/CHCL

Siku moja tu baada ya waziri wa ulinzi wa Lebanon kunadi kwamba wanamgambo wa kiislamu katika kambi za wapalestina wameshindwa kabisa,ufyatuaji risasi wa hapa na pale umesikika leo kutoka kambi za wapalestina kaskazini mwa Lebanon.

Sheikh mmoja wa kiislamu ambae akitumika mpatanishi aliarifu jana usiku kuwa wapiganaji wenye itikadi kali wa kiislamu wa kundi la FATAH ISLAM wameridhia kusimamisha mapigano na kwamba hali shuwari imerejea katika kambi ya Naher el-Bared,iliopo nje ya bandari ya mji wa Tripoli.

Lakini asubuhi ya leo ijumaa ,moshi katika sehemu 2 ulioonekana ukipaa hewani kutoka kambi hiyo huku milio ya risasi ikisikika kila baada ya muda.

Afisa mmoja wa usalama akizungumza bila kutaka kutajwa ,alisema kuwa jeshi la Lebanon linajishughulisha kung’oa na kuripua mabomu yaliozikwa na wanamgambo hao wa kiislamu.

Mapigano ya mwezi mzima sasa ya kambi ya Naher el bared ndio machjafuko makali kabisa kuikumba Lebanon kutoka ndani ya nchi tangu vita vyake vya kienyeji vya kati ya 1975-90.Machafuko ya sasa

Yamezuka katika wakati wa kinyan’ganyiro kikubwa cha madaraka baina ya serikali inayoungwamkono na nchi za magharibi ya waziri mkuu Fouad Sinora na Upinzani unaoongozwa na chama chenye itikadi kali cha Hizbollah.

Wanamgambo hao wa kiislamu wa madhehebu ya sunni wamekuwapo nchini Lebanon kwa miongo kadhaa lakini walianza kuchemka baada ya vikosi vya Syria kuihama Lebanon mwaka juzi 2005.

Itakumbukwa Machi mwaka jana,vikosi vya ulinzi vya Lebanon viliwakamata wafuasi 6 wa kissuni wa kundi hili walioungama kwamba wakipanga njama ya kumuua Sayyed Nasrallah,kiongozi wa kundi la walebanon wa madhehebu ya shiia.

August mwaka jana, Jihad Hamad,mwenye umri wa miaka 20, alijisalimisha kwa idara ya usalama ya Lebanon iliodai ameungama kushiriki katika ile njama iliozimwa na mapema ya kutaka kuripua mabomu katika magari-moshi nchini Ujerumani na kuwa ni mwanachama wa Al Qaeda.

Juzi Mei 20, polisi wa Lebanon walivamia maficho ya watu waliotiliwa shaka ni wezi wa banki mjini Tripoli,Lebanon.kitendo hiki kilichochea mapigano makali.Waliotiliwa shaka kuhusika ni wapiganaji wa kundi hilo la waislamu ambao wenzao wakajibisha kwa kuhujumu vituo vya jeshi la Lebanon kandoni mwa kambi ya wapalestina ya Naher al-Bared.

Waliwaua wanajeshi 17 wa Lebanon.

Jeshi likajibisha hujuma hapo jana na baadae likatangaza ushindi kamili mwishoni mwa changamoto kali ya siku 33.

Kwa jumla, watu 172 wameuwawa kati yao wanajeshi 76 wa Lebanon,wanamgambo 60 na raia 36 –hii ikiwa hesabu kamili ya changamoto alioitangaza jana waziri wa ulinzi.

Moshi uliochomoza leo hewani,unaacha hatahivyo, shaka shaka iwapo duru hii na wanamgambo hao wa kiislamu kweli imemalizika kabisa.