Lebanon kuwa bila ya rais?
23 Novemba 2007Lebanon inaingia katika hali isiyofahamika ya kisiasa leo Ijumaa wakati rais anayeiunga mkono Syria Emile Lahoud anaondoka madarakani huku kukiwa na hali ya kutoafikiana miongoni mwa viongozi waliogawika juu ya nani wa kuchukua nafasi yake. Upatanishi wa Ufaransa umeshindwa kufikia muafaka baina ya makundi yanayopinga na yanaunga mkono Syria kuhusiana na mtu atakayechukua nafasi ya Emile Lahoud.
Bunge lilitarajiwa kukutana leo Ijumaa kumchagua kiongozi mpya wa nchi hiyo lakini upande wa upinzani umesusia kikao hicho, na kushindwa kufikia idadi inayotakiwa ya wabunge ambao wangepiga kura ya theluthi mbili. Upigaji kura umeahirishwa kwa muda wa wiki moja hadi Novemba 30. Upinzani unaoongozwa na chama cha Hizboullah na muungano unaounda serikali unaoungwa mkono na mataifa ya magharibi wameamua kuudhibiti mzozo huo kwa kuwa na mazungumzo zaidi yenye lengo la kukubaliana juu ya rais mpya. Hii itasababisha kiti cha urais kuwa wazi hadi pale utakapopatikana muafaka. Spika wa bunge Nabi Berri , mmoja wa viongozi maarufu wa upinzani ameitisha kikao kingine hapo Novemba 30, ikiwa ni ishara kuwa sio kila kitu kimeharibika baina ya kambi hizo mbili . majadiliano yatatuwana hasa katika majina mapya kwa ajili ya kiti cha urais, nafasi ambayo imetengwa hivi sasa kwa kiongozi kutoka katika madhehebu ya kikristo ya Maronite kwa mujibu wa mfumo wa kugawana madaraka kwa makundi ya kidini nchini Lebanon.
Wakati huo huo uongozi wa serikali inayoongoza Lebanon umemtaka rais Emile Lahoud kuondoka kutoka katika jumba la rais wakati muda wake utakapomalizika usiku wa manane leo Ijumaa ama atakabiliwa na mashtaka ya uhalifu. Iwapo ataamua kubaki madarakani , itakuwa ni uhalifu dhidi ya katiba ambayo imewekwa madarakani kwa mujibu wa sheria, naibu spika wa bunge la Lebanon Farid Makari amesema , akisoma taarifa kutoka muungano wa vyama vinavyounda serikali.
Ibrahim Moussawi mhariri mkuu wa gazeti la Intaqat linalomilikiwa na chama cha Hizboullah amesema hata hivyo kuwa rais ataamua lolote kabla ya kufika muda wake wa kuondoka madarakani.
Tuna wasi wasi kuwa mzozo huu unaweza kutupeleka katika hali ya kutokuwa na rais na huenda kuigawa nchi hii. Kwa bahati mbaya sana suluhisho liko mikononi mwa mwa mataifa ya nje, hususan Marekani, amesema Ali Baaibis karani katika duka la vitu vya ujenzi. Mgawanyiko huu unaakisi mvutano wa kuwa na udhibiti nchini Lebanon baina ya Syria na Iran kwa upande mmoja , na Marekani , ikiwa pamoja na Saudi Arabia na waungaji mkono kutoka Ulaya kwa upande mwingine.