1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lavrov ziarani Mali

7 Februari 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, yuko nchini Mali kwa mazungumzo na viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo wanaosaka msaada wa Moscow kwenye kukabiliana na uasi wa makundi ya siasa kali uliodumu kwa mrefu.

https://p.dw.com/p/4NBB2
Minister Sergey Lavrov trifft  Esteban Lazo Hernandez
Picha: Russian Foreign Ministry Press Service/AP/picture alliance

Alipowasili mjini Bamako asubuhi ya Jumanne (7 Januari), Lavrov aliyetokea ziarani nchini Iraq, alipokelewa na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop.

Ziara hiyo ya chini ya siku moja ilikuwa ya tatu kwa Lavrov barani Afrika tangu mwezi Julai, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ushawishi wa Urusi kwenye bara hilo, huku ikiwa imetengwa kimataifa kutokana na uvamizi wake dhidi ya Ukraine ulioanza Februari 2022.

Tangu kuchukuwa madaraka kupitia mapinduzi yaliyofanyika mara mbili mwaka 2020, watawala wa kijeshi wanaoongozwa na Kanali Assimi Goita wamejielekeza zaidi upande wa Urusi inayowasaidia kwenye vita vyao dhidi ya makundi ya siasa kali, baada ya kuvifukuza vikosi vya jeshi la Ufaransa, mkoloni wao wa zamani.

Soma zaidi: Mali yamfukuza mkuu wa kitengo cha haki za binadamu

Tayari, maafisa kadhaa wa Mali wameshaitembelea Urusi, lakini kwa Lavrov "hii ni ziara ya kwanza ya aina yake inayodhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na usalama baina ya nchi hizi mbili," ilisema taarifa iliyotolewa na wizara ya nje ya Mali.

Mbali na kuzungumza na mwenyeji wake, Diop, Lavrov alitazamiwa kufanya mazungumzo na Goita na baadaye kwa pamoja kukutana na waandishi wa habari.

Msaada wa Urusi kwa Mali

Mali Präsident Oberst Assimi Goita
Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi Goita.Picha: Habib Kouyate/Xinhua/IMAGO

Tayari, Mali imeshapokea ndege na helikopta za kivita kutoka Moscow na pia kuna  mamia ya wanajeshi wa Kirusi - ambao viongozi wa Mali wanasema ni wakufunzi wanaosaidia kwenye masuala ya kijeshi na ulinzi wa mamlaka yake.

Maafisa wa serikali za Magharibi na baadhi ya makundi ya haki za binaadamu wanasema wapiganaji hao ni mamluki wa kampuni ya masuala ya ulinzi ya Urusi, Wagner Group, ambao wanatuhumiwa kutumia mbinu za kikatili na kuvunja haki za binaadamu kwenye maeneo mengine barani Afrika.

Soma zaidi: Wataalamu wataka vikosi vya Mali na Wagner vichunguzwe

Hata hivyo, kupitia msaada wa mamluki hao, viongozi wa Mali wanadai kupata mafanikio makubwa dhidi ya makundi ya siasa kali yaliyokuwa yakishambulia maafisa wa serikali na majengo ya umma kwa muongo mzima sasa, kwenye vita vilivyopoteza maisha ya maelfu ya watu na kuwageuza malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

Wakati mashaka dhidi ya mataifa ya Magharibi yakiongezeka kwenye baadhi ya maeneo duniani, zikiwemo nchi za Afrika, Moscow inatazamia kutumia fursa kutanuwa ushawishi wake, huku wachambuzi wakisema mataifa kadhaa ya Afrika yamekataa kulaani moja kwa moja uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. 

Chanzo: AFP