1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Lavrov: Marekani inataka kuvuruga mkutano wetu na Afrika

4 Aprili 2023

Urusi imeyatuhumu mataifa ya magharibi hususani Marekani kuwa na mipango ya kuuvuruga mkutano wa kilele kati ya Moscow na mataifa ya Afrika utakaofanyika baadae mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4Ph2Z
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Alexander Shcherbak/ITAR-TASS/IMAGO

Madai hayo yametolewa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov katika mahojiano na tovuti moja ya habari yaliyochapishwa siku ya Jumanne.

Lavrov amesema nchi za magharibi zinakula njama kuutia kiwingu mkutano huo wa kilele kwa kile inachosema kuwa sehemu ya mpango wa mpana wa nchi hizo wa kuitenga Moscow kimataifa.

Mwanadiplomasia huyo wa Urusi ameiambia tovuti ya Argumenty i Fakty kuwa Moscow ina utofauti mkubwa linapokuja suala la mahusiano yake na Afrika ikilinganishwa na nchi za magharibi.

"Sisi hatuwaelekezi washirika wetu wa Afrika jinsi wanavyopaswa kuishi. Hatuna ajenda yoyote iliyojificha nyuma ya pazia" amekaririwa kiogozi huyo wa Urusi.

Lavrov: Mipango ya mataifa ya magharibi haitotimia 

Moscow imo kwenye maandalizi ya mkutano wa pili wa kilele na mataifa ya Afrika ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi Julai huko St. Petersburg. Ajenda za kipaumbele ni pamoja na miradi ya miundombinu, teknolojia na nishati.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Afrika Kusini
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov akiwa na mwenzake wa Afrika Kusini Naledi Pandor wakati wa ziara ya Lavrov nchini Afrika Kusini mnamo Januari, 2023.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

"Ni dhahiri kwamba Marekani na washirika wake wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha Urusi inatengwa kimataifa," ameeleza Bw Lavrov. "Hususani, wanajaribu kuupiga vita mkutano wetu wa pili kati ya Urusi na Afrika ... kuwashawishi marafiki zetu wa Afrika wasishiriki."

Hata hivyo Lavrov amesema, mipango yote ya kuuharibu mkutano huo inaparaganyika kwa sababu "watu wengi wako tayari kujitenga moja kwa moja na watawala wao wa zamani wa kikoloni"

Kiongozi huyo amesema juhudi za kuingilia ushirikiano baina ya mataifa ya kusini na mashariki mwa ulimwengu zitaendelea, lakini hakuna uwezekano wa njama hizo kuzaa matunda.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani hakupatikana mara moja kujibu madai hayo mazito yaliyotolewa na Moscow.

Mapambano ya kuwania ushawishi barani Afrika yaongezeka 

Mkutano wa kilele wa Marekani na Afrika
Mkutano wa kilele kati ya Afrika na Marekani ulifanyika Disemba, 2022.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Urusi ambayo imetengwa kikamilifu na mataifa mengi ya magharibi tangu ilipoivamia kijeshi Ukraine kiasi mwaka mmoja uliopita, imehamishia juhudi zake katika kuzivutia nchi za Asia na Afrika.

Lavrov ameonesha shauku ya kutanua ushirikiano zaidi na Afrika katika miezi ya karibuni. Tangu kuanza kwa mwaka 2023, mwanadiplomasia huyo wa Urusi ameitembelea Afrika mara mbili. Ziara hizo zinafuatia nyingine aliyoifanya barani humo katikati mwa mwaka uliopita.

Ushirikiano unaotafutwa unahusisha sekta mbali mbali ikiwemo ulinzi na usalama. Mathalani, Afrika Kusini ilifanya luteka ya pamoja ya kijeshi na vikosi vya majeshi ya Urusi na China.

Hivi sasa kundi binafsi la mamluki wa kirusi la Wagner ambalo limejitwika dhima kubwa katika mapambano nchini Ukraine, limetuma wapiganaji wake pia huko Malia na Jamhuri ya Afrika ya Kati kupambana na makundi ya itikadi kali.

Kwa upande nchi za magharibi ikiwemo Marekani zimezidisha nia ya kuimarisha ushirikiano na Afrika.

Miezi michache tu iliyopita, rais Joe Biden wa Marekani aliwaalika mjini Washington viongozi wa Afrika kwa mkutano wa kilele kati ya Washington na Afrika. Marekani imekuwa na wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa ushawishi wa China.