1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Latvia yajiunga na sarafu ya Euro

Arnd Riekmann10 Julai 2013

Umoja wa Ulaya umeipitisha rasmi Latvia, kuwa mwanachama wa 18 wa kanda inayotumia sarafu ya euro. Hiki ndiyo kilikuwa kikwazo cha mwisho kwa nchi hiyo kujiunga na sarafu ya pamoja ambayo itaanza kuitumia mwakani.

https://p.dw.com/p/194tO
Waziri mkuu wa latvia, Valdis Dombrovski na waziri wa fedha, Andris Vilks Lettland.
Waziri mkuu wa latvia, Valdis Dombrovski na waziri wa fedha, Andris Vilks Lettland.Picha: Reuters

Mataifa yote matatu ya Baltic yanashika njia sawa kuelekea sarafu ya euro. Estonia tayari inatumia sarafu hiyo, Latvia nayo itaanza kuitumia mwakani na Lithuania, ambayo inashikilia urais wa baraza la umoja wa Ulaya kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu, inataka iwe imejiunga na kanda ya euro ifikapa mwaka 2015.

Sarafu ya Euro ya Latvia itakayoanza kutumika mwakani.
Sarafu ya Euro ya Latvia itakayoanza kutumika mwakani.Picha: Ģederts Ģelzis

Waziri wa fedha wa Lithuania Rimantas Sadzius anachukulia kujiunga kwa jirani yake Latvia kama ushahidi wa hilo, "kwamba ruwaza ya kiuchumi ya Umoja wa Ulaya inaweza kuishi, na hili ni muhimu si tu kwa bara la Ulaya, lakini nadhani hata kwa dunia nzima."

Waziri Mkuu wa Latvia Valdis Dombrovskis alikuja mjini Brussels kuwasilisha sarafu za euro zitakazotumiwa baadae, na alikumbuka kipindi cha giza muda si mrefu uliyopita. "Miaka michache iliyopita tulianza kusikia fununu za kusambaratika kwa kanda inayotumia sarafu ya euro, lakini sasa tunaona kuwa kanda hiyo inachukuwa hatua za kushughulikia mgogoro wa kifedha na kiuchumi, na juu ya hayo kuna imani katika kanda ya euro na kanda hiyo inapanuka," alisema waziri mkuu huyo.

Sarafu ya euro inavutia, na kwa kujiunga kwa Latvia, kanda ya euro imepokea nchi ambayo inakuwa kwa kasi kubwa na haihitaji msaada wa nje. Kinyume chake, Latvia imekuwa nchi mfadhili, na hiyo ni habari njema kwa wanachama wa sasa wa kanda ya euro.

Mafunzo kwa Kanda ya Euro

Nchi hizo nazo zinapaswa kujifunza kutokana na sera yake ya uimarishaji. Waziri wa fedha Andris Vilks anashauri hasa kuhusu kasi na makubaliano. "Maamuzi ya haraka na ya kijasiri ya wanasiasa, na mjadala mzuri wa kijamii. Laazima tuwaelezee wananchi katika mataifa yetu, nini tunapaswa kufanya ili tuwe na uchumi endelevu na wenye kushindana," alisema waziri Vilks.

Huu ni ukosoaji usio dhahiri kwa nchi kama Ugiriki, ambazo hazijajipanga vile, lakini hakuna anaesema hivyo. Siku ya Jumatatu mawaziri wa fedha wa kanda ya euro walikubali kuipatia Ugiriki fedha zaidi kutoka mfuko wa uokozi, licha ya ripoti ya wakaguzi wa pande tatu ya hivi karibuni kuonyesha matokea mchanganyiko. Kwa wakati huu, kabla ya mapumziko ya majira ya joto - na kabla ya uchaguzi nchini Ujerumani, hakuna anaependa kueneza hisia mpya za mgogoro.

Waziri Mkuu wa Latvia, Valdis Dombrovskis.
Waziri Mkuu wa Latvia, Valdis Dombrovskis.Picha: Reuters

Tatizo ni ajira kwa vijana

Lakini mwenyekiti wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda ya euro Jeroen Dijsselbloem anaona kuna hatua kubwa imepigwa. "Nadhani tumeonyesha maendeleo makubwa katika masuala mbalimbali, utulivu katika masoko ya fedha, na kurejesha imani katika sarafu ya euro, ni kweli bado tuna mengi ya kufanya kuhusu muungano wa mabenki na mageuzi ya kimuundo. Kuondoka katika mgogoro si jambo linaloweza kufanyika ndani ya miezi miwili, lakini maendeleo yako dhahiri na nadhani tunapaswa kuendelea katika njia hiyo."

Lakini waziri wa fedha wa Austria, Maria Fekter, haoni kama mabenki ndiyo tatizo kubwa kwa bara la Ulaya, bali vijana wasiokuwa na ajira. Kwa hili anataka kuwepo na juhudi zaidi. Walativia wana jibu lake. Mageuzi waliyoyafanya yameharakisha ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa ajira. Yaelekea mwanafunzi kutoka kaskazini-mashariki atakuwa na kazi ya kutoa nasaha kwa wenzake mara kwa mara.

Mwandishi: Christoph Hasselbach (DW Brüssel)
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Charo Josephat Nyiro