Löw: timu ya Ujerumani lazima ijiimarishe upya
2 Januari 2015Löw pia amethibitisha kuwa Bastian Schweinsteiger atasalia kuwa nahodha wa timu. Löw mwenye umri wa miaka 54 ameliambia shirika la habari la DPA kuwa wachezaji wake wanastahili kusalia na msingi huo mzuri lakini pia watafute mbinu mpya. Anasema lengo ni katika mwaka wa 2016 kuthibitisha mafanikio yao ya Kombe la Dunia waliyoyapata Brazil. Na ili kutimiza hilo, timu yake lazima isahau kilichotokea mwaka jana nchini Brazil.
Ujerumani wamekabiliwa na kibarua kigumu katika mechi za kufuzu katika mashindano ya Ubingwa wa Ulaya mwaka wa 2016, huku kikosi cha Löw kikiwa katika nafasi ya pili katika Kundi D na points saba kutokana na mechi nne, ikiwa ni points tatu nyuma ya viongozi wa kundi Poland.
Löw anasema lengo lake pia ni kumaliza ushindi wa Uhispania wa mataji ya Ulaya (baada ya kushinda mwaka wa 2008 na 2012) na kurudia mafanikio ya Uhispania kushinda taji la Euro baada ya kunyakua Kombe la Dunia.
Mchuano unaofuata wa Ujerumani utakuwa wa kirafiki dhidi ya Australia Machi 25 mjini Kaiserslautern. Siku nne baadaye watapambana ugenini na Georgia katika mechi yao ya kwanza mwaka wa 2015 kufuzu katika fainali za Euro. Kocha kutakuwa na mechi zitakazofuata za kufuzu dhidi ya Gibraltar, Poland, Ireland, Scotland na Georgia.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Gakuba Daniel