1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLebanon

Kwa nini Lebanon imeshindwa kuchagua rais mpya?

9 Desemba 2022

Lebanon imekuwa bila rais kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa kwa sababu wabunge wameshindwa kukubaliana kuhusu rais mpya.

https://p.dw.com/p/4KioP
Libanon  Bassam al-Sheikh Hussein Protest
Picha: Dario Sabaghi/DW

Mkwamo huo umehujumu hatua nyingi ikiwemo mageuzi ya kimfumo kuruhusu ufadhili kutoka shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) ili kuwezesha shirika la habari linalomilikiwa na serikali kutangaza michuano ya Kombe la Dunia. 

Rais Michel Aoun, mshirika wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, alimaliza muhula wake wa urais uliodumu kwa miaka sita mnamo Oktoba 30.

Tangu wakati huo, bunge la Lebanon ambalo limegawika limekutana mara tisa kujaribu kumchagua mrithi wake lakini bila mafanikio. Hali hiyio imezidisha mkwamo wa kisiasa na kuhujumu hatua za kushughulikia mgogoro wa uchumi, ambao umetumbukiza robo tatu ya raia wote nchini humo kwenye umaskini.

Vikao vya kila wiki bungeni vimekuwa kama kichekesho huku wabunge wengi wakipiga kura isiyokuwa na chaguo lolote. Wengine wanaandika kwa kejeli majina ya wanaodhani wanapaswa kuwa wagombea, likiwemo jina la marehemu Nelson Mandela wa Afrika Kusini na Salvador Allende wa Chile. Mara nyingi wajumbe hao huondoka bungeni kabla ya vikao kumalizika na kulikosesha bunge idadi inayohitajika kuendesha shughuli zake.

Rais wa zamani wa Lebanon Michel Aoun
Rais wa zamani wa Lebanon Michel AounPicha: Predency of Lebanon/AA/picture alliance

Tuhuma za kuwepo mkono wa Saudi Arabia kwenye mkwamo huo

Mkwamo huo wa kisiasa katika taifa hilo dogo, unajiri pia mnamo wakati likijaribu kufufua uhusiano wake na Saudi Arabia na mataifa mengine ya Ghuba, ambayo kwa wakati mmoja ndiyo yaliisaidia Lebanon kifedha.

Hali ya kundi la Hezbollah kutawala siasa za Lebanon katika muongo mmoja uliopita Pamoja na kundi hilo kuwaunga mkono waasi wa Kihouthi dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen, pia imeighadhabisha Saudi Arabia.

Mnamo mwaka 2021, Saudi Arabia ilipiga marufuku bidhaa za kilimo kutoka Lebanon kwa sababu meli zilizosafirisha bidhaa hizo zilidaiwa pia kusafirisha mihadarati. Baadaye mwaka huo, Saudi Arabia ilipiga marufuku bidhaa zote za Lebanon baada ya Waziri mmoja wa Lebanon kutaja vita vya Saudi Arabia nchini Yemen kuwa "upuuzi”.

Wataalam wanasema kwa sehemu fulani mkwamo huo unahusishwa na mazungumzo yanayoendelea kati ya Saudi Arabia na Iraq mjini Baghdad yanayokusudia kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia.

Je wagombea urais wa Lebnon ni kina nani?

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib MikatiPicha: Bilal Hussein/AP Photo/picture alliance

Chini ya mfumo wa Lebanon wa ugavi madaraka tangu uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1943, kwa wakati huu rais sharti atoke upande wa dhehebu la Katoliki, kwani waziri mkuu anatoka dhehebu ya Sunni na spika wa bunge anatoka dhehebu ya Shia.

Japo chama cha Hezbollah hakijatangaza rasmi mgombea wake, dhana iliyopo ni kwamba kundi hilo linamuunga mkono Sleiman Frangieh ambaye ni mshirika wa karibu wa chama hicho na pia mpambe wa rais wa Syria Bashar Assad.

Michel Moawad kutoka kambi inayopinga Hezbollah  amekuwa akipata kura zaidi ya wagombea wengine lakini ameshindwa kufikisha idadi inayokubalika ili kutangazwa mshindi.

Mkuu wa majeshi wa nchi hiyo Jenerali Joseph Aoun anapigiwa upatu pia kuwa anaweza kuwania japo jina lake halijawahi kujumuishwa miongoni mwa wagombea.

Hatma ya mkwamo huo ikiwa haijulikani, wachambuzi wengi wanasema mirengo ya kisiasa haitakuwa na budi kulegeza misimamo yao kisiasa ikiwa ni pamoja na kutenganisha uteuzi wa mawaziri na vyeo vingine vya juu serikalini.

Hage Ali, mwanadiplomasia wa nchi za magharibi ameufananisha mkwamo wa sasa na mchezo wa karata, ambapo unaficha kadi zako na kusubiri wakati muafaka wa kuzicheza na kushinda.

(APE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Mohammed Khelef