Kuzuia vazi la hijabu ni ukiukaji wa haki za binadamu
27 Februari 2009Shirika la Haki za Binadamu - Human Rights Watch, limekosoa hatua iliyochukuliwa na majimbo hayo manane kuzuia vazi la hijabu.Katika ripoti iliyotolewa mjini Berlin shirika hilo limesema,huo ni ubaguzi wa wanawake wa Kiislamu.
Mdahalo wa vazi la hijabu ulizuka nchini Ujerumani mwishoni mwa miaka ya 1990, pale mwalimu wa Kiislamu kutoka Afghanistan, Fereshta Ludin aliposhikilia kujifinika kichwa kwa mtandio wakati wa kusomesha licha ya kukatazwa na mkuu wa shule hiyo.Hatimae mwalimu huyo alikwenda hadi Mahakama ya Katiba ya Ujerumani mjini Karlsruhe na mwaka 2003 mahakama hiyo ikaamua kuwa walimu wa Kiislamu hawawezi kukatazwa vazi hilo darasani bila ya kuwepo msingi wa kisheria.Lakini ikathibitisha kuwa kisheria,majimbo yana haki ya kupitisha sheria kama hiyo kuzuia vazi la hijabu.
Hatimae,sheria za shule katika majimbo manane zilibadilishwa ili kuweza kuwazuia walimu kuvaa hijabu darasani.Katika baadhi ya majimbo hata wafanyakazi katika ofisi za kiserikali hawaruhusiwi kujifunika kichwa kwa hijabu.Majimbo mengine manane hayana sheria kama hiyo.
Ripoti ya Human Rights Watch imetolewa baada ya kufanywa uchunguzi mbali mbali katika mwaka 2008.Jumla ya watu 72 katika majimbo tofauti ya Ujerumani na hata wanasiasa,wanasayansi na wajumbe wa taasisi na mashirika yasio ya kiserikali walihojiwa.Miongoni mwao, walikuwepo wanawake 34 wa Kiislamu wanaoishi Ujerumani na ambao wameathirika kwa sababu ya sheria inayowazuia kuvaa hijabu.
Kwa mujibu wa mwanasheria Haleh Chahrokh wa Human Rights Watch, maisha ya wanawake hao yamebadilika.Baadhi yao hawakurejea kazini baada ya kumaliza kipindi cha mapumziko ya uzazi.Na wengine wamehamia majimbo mengine au hata nchi zingine.Lakini wapo waliohisi kuwa hawana chaguo jingine isipokuwa kuivua hijabu ili kuweza kubakia kazini.Wanawake hao wanahisi kama wamepotoshwa na sheria hiyo kwa sehemu fulani.
Shirika la Human Rights Watch limetoa mwito kwa majimbo yanayopiga marufuku mavazi au alama za kidini kubatilisha sheria hiyo. Limesema,serikali za majimbo zinapaswa kuhakikisha kuwa sheria zake hazibagui jinsia au dini na zinaheshimu uhuru wa dini na maoni.