Kuwarejesha Waafghanistan ni kinyume na haki za binadamu
6 Oktoba 2017Hii ni kinyume na sheria anaeleza mtafiti wa shirika hilo la haki za binadamu Horia Mosadiq katika mahojiano yaliyofanywa na Jawad Amanullah wa DW.
Ripoti ya hivi karibuni kabisa ya Amnesty International inasema kuwa watu nchini Afghanistan wanakabiliwa na matumizi ya nguvu, kutekwa nyara na mauaji. Ni hali mbaya kiasi gani inalikumba jimbo la Hindukush? aliulizwa mtafiti huyo Horia Mosadig, ambaye amesema, hakuna usalama nchini Afghanistan.
Ametoa mfano kwamba, alitekwa nyara baba mmoja wa familia na watu waliokuwa na silaha, na familia yake ikalazimika kukusanya fedha zao za mwisho ili kumkomboa mzee wao. Baada ya hapo familia hiyo ilikimbilia Norway na kuomba hifadhi ya ukimbizi.
Wakiwa nchini Norway ombi lao la hifadhi ya ukimbizi lilikataliwa. Wakalazimika kurejeshwa nchini Afghanistan. Miezi michache baadaye baba huyo alipotea tena. Lakini siku chache baadaye mwili wake ulionekana mjini Kabul akiwa amekufa. Wakimbizi hao kwa mujibu wa maafisa walirejea kwa hiari yao kutoka Ulaya. Wanapaswa kutambua kuwa kuna hatari katika nchi zao.
Hadi leo kuna Waafghanistan 9,000 waliorejeshwa nchini humo kutoka Ulaya. Wengine 80,000 wako katika hatari ya kurejeshwa. Mataifa ya Ulaya yanaonesha kwamba kurejea kwa Waafghanistan nchini mwao ni kwa hiyari. Lakini ukweli ni kwamba si kwa hiyari. Wakimbizi wa Afghanistan wanaelezwa, kwamba kwa njia moja au nyingine watarejeshwa tu makwao na kuna aina mbili tu ya uwezekano. Ama warejeshwe bila kupewa msaada wowote, ama watie saini fomu ya kurejeshwa na wapatiwe msaada wa serikali, ili kujenga maisha yao mapya nchini Afghanistan.
Wakimbizi wa Afghanistan
Ni Mataifa gani huwarejesha zaidi wakimbizi wa Afghanistan makwao. Ujerumani ni moja kati ya nchi hizo, ikifuatiwa na Ugiriki, Norway, Sweden na uingereza. Pamoja na hayo nchi zote karibu za Ulaya huwarejesha wakimbizi wa Afghanistan makwao. Anmesty International imesema inafanya mazungumzo na nchi hizi zote za Ulaya pamoja na Afghanistan yenyewe. Mahitaji yetu kwa nchi za Ulaya , ni kwamba zisichukue tena hatua za kuwarejesha wakimbizi wa Afghanistan. Kwa upande wa serikali ya Afghanistan tunatarajia , kwamba zisitoe msaada ili kuweza wakimbizi hao kurejeshwa nchini humo.
Kuhusu msingi gani ambao unatumiwa na mataifa ya Ulaya kuwarejesha wakimbizi hao, mtafiti wa Amnesty International Horia Mosadiq anasema, ni vigumu kuweza kupambanua vipengee vya uamuzi huo. Lakini hatua ambayo inaleta wasi wasi mkubwa, ni kwamba idadi ya kukataliwa maombi katika mataifa ya Ulaya imepanda mno hivi karibuni, hususan tangu mwezi Februari ambapo serikali ya Afghanistan ilipotia saini makubaliano kuhusu wakimbizi na Umoja wa Ulaya.
Hadi leo haijakuwa wazi, ni jimbo gani katika Afghanistan ni salama, na lipi si salama. Bado hali haifahamiki katika mataifa ya Ulaya.
Wakimbizi mashoga
Tunafahamu kutoka kwa wakimbizi wenyewe, amesema mtafiti huyo wa Amnesty International , kwamba kwa wale waliotoa sababu ya kwamba wao ni mashoga ili kuomba hifadhi , pia wanarejeshwa. Hata waliobadili dini na kuwa Wakristo na wengine wengi ambao wanafuatiliwa nchini Afghanistan kutokana na msimamo yao ya kisiasa ama kidini, hawana msaada katika mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Majimbo kama Kabul, Panjshir, Bamyan yanaonekana kuwa yana usalama. Lakini huo sio ukweli ulivyo. Kabul kwa mfano ndio mji mkuu wa Afghanistan, na ndiko kunakotokea mashambulizi mara kwa mara. Hatukubaliani katika swala hili na kile mataifa ya Ulaya yanachofanya. Nchini Afghanistan hakuna kanda ambayo ina usalama, na hakuna eneo , ambalo unaweza kuwarejesha wakimbizi. Nchi ambazo zinachukua hatua ya kuwarejesha wakimbizi zinakwenda kinyume na haki za binadamu.
Mwandishi: Amanullah, Jawad / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo