1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuvuja kwa mionzi ya nyuklia yawa mada kuu Ujerumani

14 Machi 2011

Tahriri za magazeti ya hapa Ujerumani leo hii (14.03.2011)zimetawaliwa na kitisho kinachovikabili vinu vya nyuklia nchini Japan, ikikumbukwa pia kuwa Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yanayotumia nishati hiyo.

https://p.dw.com/p/10Yjp
Athari za tetemeko nchini Japan
Athari za tetemeko nchini JapanPicha: dapd

Mhariri wa gazeti la Rheinische Post anasema, ikiwa kuna somo lolote ambalo Ujerumani inaweza kujifunza kutoka maafa haya ya Japan, ni kwamba wakati wa kuvifunga vinu vyake vya nyuklia sasa umefika.

Hofu ya mhariri ni kuwa kuna miaka mingine 999,975, ya kuishi na hofu na wasiwasi kwamba kuna siku miyale ya nyuklia itavuja kutoka vinu vyake, na kuzagaa.

Na sababu ni kuwa, hakuna anayeweza kuhakikisha usalama wa moja kwa moja wa nishati hii yenye madhara makubwa kwa wanaadamu na mazingira.

Mhariri huyo anasema: haisadii kitu kukimbilia kuwasaidia watu wanaokabiliwa na hatari ya mionzi ya nyuklia kwa wataalamu na pesa tu. Inasaidia zaidi kuzuia uwezekano huo usitokee. Nako ni kuzimaliza hizi siasa za atomiki. Vyenginevyo, muda wa kuvuta hewa safi duniani unapungua, na uamuzi tunao mikononi mwetu.

Suala jengine lililoshugulikiwa na wahariri ni lile la sarafu ya Euro, ambapo mwisho wa wiki iliyopita, viongozi wa eneo linalotumia sarafu hiyo walikubaliana kuwa na uratibu wa pamoja wa sera za kiuchumi kwenye mataifa yao.

Lakini mhariri wa gazeti la Westfallen-Blatt anasema kuwa maneno ya wanasiasa hayaaminiki. "Ahadi za wanasiasa ni matamshi kwenye makaratasi tu, si lazima zitekelezwe". Ndivyo anavyosema mhariri huyo.

Alichoweza kufanikisha Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kufikiwa mjini Brussels, na ambacho hivi sasa kimo kwenye makaratasi, si kibaya sana.

Nchi zinazotumia sarafu ya Euro zinatoa ruhusa ya kila mmoja kuwa na usemi kwa mwenzake, panapohusika na sera kuu za uchumi, lengo likiwa, ni kufikia pahala ambapo pana nidhamu ya fedha. Makubaliano yanahusiana na masuala ya pesheni, kodi, mikopo na, kwa hivyo, upunguzaji wa ajira zisizo na tija kwa taifa.

Lakini suali ni: je ni kweli haya yanatekelezeka, panapohusika nchi zinazotumia safaru moja, lakini zenye tafauti kubwa za kiuchumi ndani yake?

Mwisho ni mkasa wa mwishoni mwa wiki huko kwenye makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ambako mtu anayeshukiwa kuwa ni Mpalestina alifanya mauaji ya maangamizi kwa familia nzima ya Kiyahudi, akiwaua kwa kisu baba, mama na watoto wao watatu.

Mhariri wa wa gazeti la Neue Osnabrücker anasema, hakuna mtu anayeweza kudai kuwa mauaji haya ya kikatili yalichochewa na maslahi ya kisiasa. Na wala si lazima iwe ni muuaji yaliofanywa na Mpalestina. Maana wakiwa wanaishi kiuhasama na jamii za Kiarabu zilzowazunguka, Wayahudi wanaweza kufanyiwa jambo hili na yeyote miongoni mwa majirani hao.

Lakini kilicho wazi ni kuwa Israel inapaswa kuhakiki upya siasa zake katika eneo hili, hasa hili la ujenzi wa makaazi ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA
Mhariri: Othman Miraji