Kutawazwa kwa Obama
21 Januari 2009Maoni ya wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani, yamejishughulisha takriban na mada moja tu:Tukio la historia la kutawazwa Barack Hussein Obama, rais wa 44 wa Marekani akiwa Mmarekani wa kwanza wa asili ya kiafrika kushika wadhifa huo: Gazeti la Badisches Tagblatt laandika:
"Raia wa marekani kwa kumchagua Obama wametoa ishara.Kwanza, kabisa ishara hiyo ni kuwa sio tu jamii za wachache nchini Marekani ziwe na tamaa,bali kuwaonyesha wanadamu kote ulimwenguni , kwamba dola kubwa ulimwenguni sio tu limeshakomaa kufanya mageuzi,bali linaweza kuyafanya mageuzi hayo binafsi.
Gazeti la Heilbronner Stimme limeandika:
"Wamarekani, wamekuwa na desturi ya kuandaa sherehe kubwa za kuapisha rais wao mpya.Lakini mara hii, zilitia fora zaidi.Kama ilivyo onekana nyakati za kampeni ya uchaguzi,shangwe na shauku ya wananchi mjini Washington,Marekani nzima na hata kote ulimwenguni, zilisisimua mno.Pekee, hii inamfanya rais huyu kuingia katika historia."
Westfalische Nachrichten kutoka mji wa Munster limeandika:
"Ulimwengu umebadilika na sisi yatupasa pia kubadilika.Hiyo ndio risala muhimu kabisa alioitoa Barack Obama katika hotuba yake ya kutawazwa kuwa rais wa Marekani.........Obama aliwapasulia wamarekani wazi wazi kwamba, wanajikuta kati kati ya msukosuko mkubwa wa kiuchumi na kwamba miezi ijayo itakuwa migumu.
Ndio maana aliwataka wamarekani kurejea katika desturi zao za kale."
Ama gazeti la Badische Zeitung kutoka Freiburg, lakumbusha kwamba ,mzigo wa madeni wa mabilioni ya dala,msukosuko mkubwa wa uchumi tangu kupita miaka 80,vita visivyomalizwa nchini Irak na Afghanistan ,nadra kwa rais kuanza kazi yake akikabiliwa na hali ngumu kama hiyo. Gazeti lasema:
"Lakini,kueneza furaha,kupalilia matumaini na kuwakumbusha raia jukumu lao,hakutatosha kuwa turufu pekee ya kisiasa kutatua matatizo yaliopo..."
Mwishoe,gazeti la Mitteldeutsche Zeitung kutoka Halle linatumalizia kwa kuuliza:
"Ilikuaje mwanasiasa huyu akaekewa matumaini makubwa namna hii ?
"Kuna majibu mengi ya swali hili.Matarajio yaliorundikana hadi mwishoni mwa utawala wa George Bush, bila ya shaka yamechangia nayo mno. Kwa upande mwengine, ni heba yake binafsi Obama inayowavutia watu na kumwekea matumaini yao."