1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kurudi kwa Zuma urais ANC

21 Desemba 2012

Maoni kutoka DW Bonn yanatafuta majibu ya kilichoisukuma ANC kumrudisha tena madarakani kiongozi anayekosolewa vikali sio tu kwa kushindwa kudhibiti ufisadi na ghasia lakini pia mwenye kashfa kadhaa za kibinafsi.

https://p.dw.com/p/177aO
Rais Jacob Zuma.
Rais Jacob Zuma.Picha: Stephane de Sakutin/AFP/Getty Images

Je, chama hiki kilichoasisiwa miaka 100 iliyopita kwa lengo la kumkomboa Mwafrika kutoka mikono ya utawala wa kibaguzi kimefanikiwa kweli kumkomboa Mwafrika huyo hata baada ya kuwa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili sasa? Au nacho kimejigeuza kuwa cha "kikaburu" kwa namna yake yenyewe chini ya viongozi akina Zuma?

Vipi kuhusu kuingia tena kwenye nafasi ya ngazi za juu mfanyabiashara na milionea, Cyrill Ramaphosa, ambaye mkutano huo mkuu wa ANC ulimchagua kuwa makamu rais wa Zuma?

Je, kuchaguliwa tena kwa Zuma na Ramaphosa kulikusudiwa kutowe ujumbe wowote maalum kwa Afrika Kusini au ilikuwa suala la sadfa tu?

Kurudi kwa Ramaphosa na athari zake

Wako wanaodhani kuwa tukio kubwa hasa haikuwa kuchaguliwa tena kwa Zuma, bali ni kurudi tena kwenye ulingo wa kisiasa kwa Ramaphosa, ambaye kwa zaidi ya miaka 10 alikuwa amejitenga kando na siasa na kushughulikia biashara zake. Hivi kipi kilichomo kwenye uwezo binafsi wa Ramaphosa, kama kiongozi ndani ya ANC inayojikurubisha kwa Waafrika masikini?

Kuna pia suala la kuendelea kubakia kwa falsafa ya ukombozi ndani ya damu ya ANC. Afrika Kusini ni taifa kubwa sana kiuchumi barani Afrika. Kwa hakika, hata kwenye ngazi ya kilimwengu, ina nafasi yake. Ni mmoja wa wanachama wa lile kundi linaloitwa BRICS, lenye masoko yanayoinukia kiuchumi duniani. Lakini ni Afrika Kusini hiyo hiyo, chini ya utawala wa ANC, inatajwa kwamba Mwafrika wa kawaida, bado amekuwa yule yule wa kabla ya utawala wa walio wengi.

Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na Makamu wake, Kgalema Motlanthe.
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na Makamu wake, Kgalema Motlanthe.Picha: Reuters

Miaka 18 baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, bado nchi hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa mataifa yasiyo na usawa duniani na pia yenye umasikini. Watoto milioni 19, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF, wanaishi kwenye umasikini wa kupindukia.

ANC na umasikini wa Waafrika ya Kusini

Watoto wanne katika kila 10 wanaishi kwenye nyumba ambazo hakuna hata mwanafamilia mmoja mwenye ajira. Watoto 330,000 na watu wazima milioni tano ni waathirika wa ugonjwa hatari wa Ukimwi, amabo asilimia 40 kati yao hufa kwa magonjwa yatokanayo na Ukimwi. Wengi wao ni wa wale wale Waafrika weusi waliopigania kuuondosha utawala wa kikaburu.

Kiongozi muasi wa ANC, Julius Malema.
Kiongozi muasi wa ANC, Julius Malema.Picha: Reuters

DW inauliza hili linatoa ujumbe gani kwa taifa kubwa la Afrika ya Kusini, tajiri pia kama yalivyo mengine kwa rasilimali zake, lakini zaidi likiwa na uongozi ulioonja machungu ya umasikini, ubaguzi na kutawaliwa?

Je, kile ambacho kimekuwa kikiyakumba mataifa ya Afrika baada ya uhuru, yaani kupotea kwa njozi za wananchi kufaidika na keki ya taifa, ndicho kile kile kinachoikumba Afrika ya Kusini, na kwa hivyo miaka mingine 30 ijayo nayo itakuja kutembea na kibakuli cha kuombea kwenye mataifa tajiri, mithali ya leo zifanyavyo nchi zilizopata uhuru wake miaka 50 nyuma?

Katika wakati ambapo matokeo ya kura ya maoni yaliyochapishwa hapo Afrika ya Kusini mara tu baada ya kutangazwa kwa Zuma kurudi tena kwenye urais wa ANC, yanaonesha kwamba anaungwa mkono na kiasi cha asilimia 52 tu nchini kote, ikiwa ni tafauti na asimilia 70, ambacho kilimuunga mkono Kgalema Motlante, aliyekuja kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho, DW inauliza je, hii inamaanisha kwamba si umaarufu wa Zuma uliompa kura, bali ni uamuzi wa Montlante kujitoa, na hivyo Zuma ana wakati mgumu sana kujiuza yeye mwenyewe kwa wapiga kura wa Afrika ya Kusini?

Uasi ndani ya ANC?

Na mwisho, DW inauliza kuhusu hatima ya ANC ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo katika wakati ambapo kundi la vijana ndani ya ANC likiongozwa na Julius Malema, ambaye amefukuzwa kutoka uongozi wa tawi la vijana la chama hicho, linaaamini kwamba uongozi wa makomredi wa ANC umefeli na unaifelisha Afrika ya Kusini, ambayo vijana wake wengi hawana kumbukumbu za utawala wa kibaguzi, bali wanataka kuishi kwenye ahadi za ANC iliyopigania kuondosha ubaguzi.

Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe.
Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe.Picha: picture-alliance/dpa

ANC inaonekana si moja tena, kama ilivyowahi kuwa hapo kabla. Ukichukulia migomo kwenye sekta ya madini na usafiri ya hivi karibuni, mauaji ya wachimbaji madini, kashfa za ufisadi na za binafsi za Zuma mwenyewe. Je, kuna dalili yoyote ya kuibuka kwa mbadala wa ANC kwenye utawala ndani ya kipindi kifupi kijacho?

Mohammed Khelef anaongoza mjadala juu ya masuali hayo na mengine unaowashirikisha Prof. Mwesiga Baregu, ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Tanzania; Gwandumi Gwappo Atufwene Mwakatobe, mwandishi na mchambuzi wa siasa za Afrika anayeishi Mbeya, Tanzania na mwandishi wa habari Isaac Khomo wa Pretoria, Afrika ya Kusini.

Kusikiliza kipindi hiki, tafadhali bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.

Makala: Maoni
Mtayarishaji: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo