Kura zahesabiwa baada ya uchaguzi wa bunge Tunisia
27 Oktoba 2014Ikiwa bado kura za uchaguzi wa Bunge zinaendelea kuhesabiwa nchini Tunisia kufuatia uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili (26.10.2014), hadi sasa chama cha upinzani kisichoegemea dini cha Nidaa Tounes kimeshinda viti zaidi ya 80 dhidi ya chama tawala cha Ennahda kilichojipatia viti 67. Uchaguzi huu ni wa pili tangu kushuhudiwa vuguvugu la mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011.
Tume ya uchaguzi inatarajiwa kutangaza rasmi matokeo baadae leo, lakini chama cha kiislamu cha msimamo wa wastani cha Ennahda kinaonesha dalili za kupoteza nafasi yake ya uongozi. Chama hicho kimeiongoza serikali ya muungano ya Tunisia baada ya kushinda viti vingi zaidi katika uchaguzi wa mwaka 2011 kufuatia kuangushwa madarakani kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Zine el-Abidine Ben Ali.
Viongozi wa chama cha Ennahda wametoa wito Jumapili kwa wafuasi wao kusubiri matokeo rasmi, wakati kiongozi wa chama cha upinzani cha Nidaa Tounes Beji Caid Essebsi alisema dalili zinazoonekana ni kuwa chama chake kinaongoza katika uchaguzi huo.''
Kiongozi huyo aidha alisema, "Kwa kweli kuna viashiria vingi vinavyonesha kwamba Nidaa Tounes, Mungu akipenda , tutakuwa katika nafasi ya kwanza. Hatuwezi kuzungumzia matokea kutangazwe matokeao rasmi. Hata hivyo kuna viashiria vingi vinavyotupa furaha mpaka sasa. Tunasubiri matokeo ya mwisho ili kutoa maoni yetu."
Tume ya uchaguzi inatarajiwa kutangaza matokeo ya awali baadaye leo, lakini vyama vikubwa vina mawakala wake katika kila kituo cha kupigia kura kusimamia zoezi la kuhesabu kura.
Uwezekano wa kuundwa serikali ya mseto
Kwa hakika hakuna chama kinachotarajiwa kushinda moja kwa moja, ila kinachosubiriwa ni kupatikana kwa maamuzi ya kuunda serikali mpya ya muungano.
Tangu maandamano yaliyopelekea kutokea kwa mapinduzi mwaka 2011, Tunisia imeonesha utulivu tofauti na nchi jirani za kiarabu za Afrika Kaskazini ikiwemo Misri,na Libya. Hata hivyo, masuala kama kukosekana kwa ajira, fursa za kiuchumi na kuwepo kwa migogoro ya chini kwa chini na makundi ya wanamgambo wa kiislamu, yameiweka Tunisia katika hali ya wasiwasi hasa kwa vile uchumi wa nchi hiyo unategemea sana utalii wa kigeni.
Uchaguzi wa bunge jipa uliofanyika Jumapili ni hatua ambayo huenda ikaleta demokrasia kamili ndani ya nchi hiyo miaka minne baada ya kutimuliwa madarakani raisi wa zamani Ben Ali kufuatia vuguvugu la maandamano ya yakudai demokrasia yaliyoibuka pia kwenye nchi nyingine kadhaa za kiarabu kwenye eneo la Afrika Kaskazini.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/RTRE
Mhariri: Saumu Yusuf Ramadhan