Kura zaanza kuhesabiwa Nigeria
23 Februari 2019Kura hizo zinahesabiwa huku tume ya uchaguzi ikiwa imeongeza muda wa kupiga kura katika baadhi ya vituo vya kupiga kura kutokana na kuchelewa kufunguliwa kwa vituo hivyo au baadhi ya mashine za kupigia kura kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Wakizungumza baada ya kupiga kura, Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na mpinzani wake mkuu mfanyabiashara Atiku Abubakar wote wamesema wana uhakika wa kushinda. ''Hadi sasa mambo ni mazuri. Nitajipongeza mwenyewe. Nitaibuka mshindi,'' alisema Buhari wakati akizungumza na waandishi habari.
Buhari ambaye anagombea muhula wa pili madarakani, katika kinyang'anyiro hicho cha kuliongoza taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika amepiga kura katika mji alikozaliwa wa Daura, jimbo la kaskazini la Katsina, Atiku akipiga kura yake Yola, mji mkuu wa jimbo la Adamawa.
Afisa wa ngazi ya juu wa Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria, INEC, Festus Okoye, amesema upigaji kura tayari umekamilika kwenye baadhi ya maeneo na hatua ya kuhesabu kura imeshaanza. Okoye amesema tume hiyo imeongeza muda kwenye baadhi ya vituo vya kupiga kura ambavyo vilichelewa kufunguliwa.
Amebainisha kuwa wanayashughulikia matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kama vile dosari katika shughuli nzima ya uchaguzi, ikiwemo masuala ya usalama. ''Tunajaribu kuyashughulikia matatizo haya na tuna uhakika kwamba tutafanikiwa,'' alisema Okoye.
Matokeo kutangazwa wiki ijayo
Matokeo ya uchaguzi huo ulioahirishwa saa chache kabla ya vituo vya kupiga kura havijafunguliwa Jumamosi iliyopita, yanatarajiwa kutolewa mapema wiki ijayo, ambapo mshindi ataiongoza Nigeria katika kipindi cha miaka minne. Muda mfupi kabla vituo vya kupiga kura havijafunguliwa, mwanajeshi mmoja aliuawa na wengine 20 walijeruhiwa baada ya kundi la Boko Haram kuushambulia mji wa Maiduguri, ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Vikosi vya usalama na wakaazi wa eneo hilo wamesema milipuko kadhaa ilisikika katika mji wa Maiduguri, jimbo la Borno, ambako makundi ya Boko Haram na linalojiita Dola la Kiislamu IS kanda ya Afrika Magharibi yamekuwa yakifanya mashambulizi kwa muongo mzima.
Msemaji wa jeshi, Kanali Musa Sagir amethibitisha kuwa shambulizi la Geidam, nyumbani kwa gavana wa Yobe, limetokea majira ya saa 12.30 asubuhi kwa saa za Nigeria.
Mapigano pia yameripotiwa kwenye miji ya Auno na Goniri, kwenye pande zote za mpaka kati ya majimbo ya Borno na Yobe, huku shambulizi jingine la roketi likiwa limefanywa kwenye mji wa Gwoza.
Zaidi ya Wanigeria milioni 84 waliandikishwa kupiga kura katika uchaguzi wa taifa hilo la Afrika Magharibi lenye wakaazi milioni 190, lakini ni raia milioni 72.8 ndiyo wana haki ya kupiga kura, idadi hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 86. Wananchi hao pia wanawachagua wabunge.
Mwandishi: Grace Paricia Kabogo/AFP, DPA, AP, Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid