1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura maoni juu ya katiba yafanyika Myanmar

Mohamed Dahman10 Mei 2008

Myanmar yafanya kura ya maoni na kupuuza wito wa jumuiya ya kimataifa kutaka iahirishwe ili kushughulikia zaidi juhudi za kuwapatia misaada ya dharura wahanga wa kimbunga kilichopiga mji mkuu wa nchi hiyo Yangon.

https://p.dw.com/p/Dxmt
Licha ya kimbunga kuleta uharibifu mkubwa nchini Myanmar na kusababisha maafa utawala wa kijeshi umendeleea na kura ya maoni juu ya katiba.Picha: AP

Kura ya maoni inaendelea kufanyika juu ya katiba iliopendekezwa na utawala wa kijeshi nchini Myanmar kama sehemu ya mpango wa kurudisha demokrasia nchini humo.

Mapema jumuiya ya kimataifa imeutaka utawala huo wa kijeshi kuahirisha kura hiyo ya maoni na kuzipa umuhimu jitahada za kufikisha misaada kwa zaidi ya wahanga milioni moja wa kimbunga kilichopiga nchini humo Jumamosi iliopita.Huo ni uchaguzi wa kwanza nchini Myanmar kuwahi kushuhudiwa kwa zaidi ya muongo mmoja na kura hiyo ya maoni inafanyika katika maeneo yote isipokuwa yale yalioathiriwa vibaya na kimbunga nchini humo.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa imeomba msaada wa dharura wa dola milioni 120 kusaidia wahanga wa kimbunga hicho.

Utawala wa kijeshi wa Myanmar umesambaza msaada huo wa kimataifa lakini umebandika majina ya magenerali waandamizi kwenye shehena ya msaada huo katika kile kinachojidhihirisha kuwa juhudi za kugeuza juhudi hizo za msaada kuwa zoezi la propaganda.

Televisheni ya taifa imekuwa ikiendelea kuonyesha magenerali wandamizi akiwemo kiongozi wa utawala wa kijeshi Generali Than Shwe akikabidhi maboksi ya misaada kwa wahanga.