1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuporwa mali asili ya Jamhuri ya Kidimokrasi ya Kongo

Miraji Othman5 Januari 2006

Ripoti iliyotolewa mwaka jana na shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za binadamu-HUMAN RIGHTS WATCH lenye makao yake makuu nchini Marekani, imetahadharisha kuwa Uganda huuza dhahabu yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 60 kwa mwaka, wakati ambapo nchi hiyo ina uwezo wa kutoa dhahabu yenye thamani ya dola za kimarekani elfu 25 tu.

https://p.dw.com/p/CHo3
Mgodi wa almasi nchini Kongo
Mgodi wa almasi nchini KongoPicha: AP

Uchimbaji haramu wa dhahabu katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo unatokana na migogoro ya kisiasa nchini humo, na ni kikwazo cha juhudi za kutafuta amani ya kudumu mashariki mwa Congo na katika eneo lote la Maziwa Makuu.

Makundi mbali mbali huko mashariki ya Congo bado yanagombania utawala wa eneo hilo lenye utajiri wa madini ingawa eneo hilo limeathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokwisha mwaka 2002.

Awali, umoja wa mataifa ulitaka kuzua mjadala ambao ulizishutumu nchi za Uganda na Rwanda, kwamba zinapora kiasi kikubwa cha madini kutoka Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Wakati wa vita vya miaka mitano vya wenyewe kwa wenyewe nchini Congo, Uganda na Rwanda pia zilikuwa zikiyaunga mkono baadhi ya makundi katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo. Nchi zote mbili zilichukulia suala la usalama kuwa kigezo cha kuwepo kwao nchini Congo.

Rwanda inasema kuwa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, yaliingiza nchi hiyo kwenye wakati mgumu na shida.

Wahutu wenye siasa kali ambao walisaidia kuendesha mauaji ya halaiki nchini Rwanda mnamo mwaka 1994, walikimbia hadi Congo, wakati huo ikiitwa Zaire, na waasi wa ki-Tutsi wakachukua madaraka ya kuitawala nchi hiyo mwaka huo huo. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa wanyarwanda kuivamia Congo mwaka 1996 na kupelekea kuangushwa kwa aliyekuwa kiongozi wa Zaire,Mobutu Sese Seko.

Ripoti ya wataalamu wa umoja wa mataifa ya mwaka 2001, imebainisha kuwa marais Yoweri Museveni wa Uganda, na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame wanakaribia kuwa kama washirika wakuu katika kupora mali za asili za Congo.

Pamoja na yote hayo, baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo wa madini nchini Congo katika eneo la Mongbwalu lililopo Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo, wanasema wanapata karibu dola za kimarekani 150 kwa mwezi kwa kuuza chembechembe za dhahabu. Wanaiuza dhahabu hiyo kwa wafanyabishara wadogo, halafu inakuwa chini ya uangalizi wa wanamgambo na inasafirishwa kupitia Ziwa Edward kwenda kwa wafanyabiashara nchini Uganda.

Tunafahamu kwamba dhahabu ya nchi yetu inakwenda Uganda, lakini tujali nini? Serikali yetu haitujali’, alisema Floriment Fonema wa huko Mongbwalu- Congo.

Mwaka 2006 ukiwa umeanza, biashara haramu ya dhahabu, chuma, almasi, mbao na madini mengineyo inaendelea, huku wanunuzi wa malighafi hizo watokao barani Ulaya na Kusini Mashariki mwa Asia wanadai wamezinunua kutoka Uganda na Rwanda.

Dhahabu yetu ina laana. Nimepoteza ndugu zangu wakati wanamgambo wakigombea dhahabu, na sasa inabidi nichimbe dhahabu ili niweze kuishii,’ alisema Pascal Kalabo, mchimbaji wa madini huko Congo.

Mfanyabiashara wa kihindi kwenye eneo la Mongbwalu, David Dhal, anasema mzunguko wa biashara ya dhahabu ya Congo umepangiliwa kwa umakini mkubwa, na wasimamizi wake ni wafanyabiashara wakubwa walio nchi za nje, ambao wanawatumia mawakala waliopo Congo kuipata dhahabu hiyo.

Kwa mujibu wa wachunguzi katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo, kutakuwa na mbinyo mdogo wa kuwazuia watu wa mataifa mbalimbali kununua madini hayo kwa njia ya biashara haramu,hadi pale wanasiasa wenyewe wa Congo, ambao baadhi yao wanatuhumiwa kujinufaisha na biashara hiyo haramu, watakapolichukulia hatua tatizo hili.

Rahab Fred