Kuondoka kwa majeshi ya Magharibi Afghanistan kutasababisha maafa
15 Septemba 2009Kuyaondoa mapema majeshi ya mataifa ya Magharibi nchini Afghanistan kutasababisha maafa makubwa katika eneo hilo, maafisa wa nchi za Magharibi na Afghanistan wamesema, wakizungumzia kuhusu ongezeko la mapigano yanayofanywa na wanamgambo.
Hali ya juu ya kutokuwa na usalama itasababisha nchi za Magharibi kuhitajika kuingilia kati zaidi katika maeneo ambayo ni pamoja na Pakistan yenye silaha za nyuklia na kupambana na kundi la al-Qaeda. Maafisa hao wanasema kwamba hakuna njia mbadala ya kujihusisha kwa hivi sasa ambayo itaruhusu kupunguza majeshi katika muda fulani wakati nchi hiyo inapata uthabiti.
Wakati ghasia za wapiganaji zikiendelea tangu kundi la Taliban lilipoondolewa madarakani mwaka 2001, uungwaji mkono vita hivyo na wananchi unapungua nchini Marekani, na umeporomoka kabisa katika bara la Ulaya. Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Pakistan, Hilary Synnott, akizungumza katika mkutano hivi karibuni mjini Geneva uliowahusisha wataalamu wa kupanga mikakati, uliotayarishwa na taasisi ya kimataifa ya Uingereza kuhusu taaluma ya kupanga mikakati, alisema wakosoaji wa mikakati wa nchi za Magharibi lazima waangalie matokeo makubwa ya kile kinachoonekana kuwa ni kushindwa Marekani. Synnott alisema kuna wasiwasi mkubwa juu ya Pakistan ikiwa ina kiasi mara tano ya idadi ya watu nchini Afghanistan na ambayo ina silaha za nyuklia na pia ina kitisho kipya cha Taliban wa Pakistan, ikilitishia taifa hilo. Sherard Cowper-Coles, mwakilishi maalum wa Uingereza nchini Afghanistan na Pakistan, amewaambia wajumbe kuwa wale wanaodai kama baadhi yao kwamba werevu ni kujitoa kutoka Afghanistan kutaharibu kila kitu kilichokwishapatikana.
Mohammad Masoom Stanekzai, mshauri wa Rais Hamid Karzai katika masuala ya usalama wa ndani ya nchi na upatanishi, alisema kuwa gharama za kujiondoa kwa majeshi hayo itakuwa kubwa zaidi kuliko gharama zinazotumika kwa sasa. Kuondoka kwa haraka itakuwa makosa yale yale kama vile Marekani ilivyojitoa katika eneo hilo miaka ya 1990 baada ya kujitoa kwa iliyokuwa Urusi ya zamani, ambapo upengo hilo lilisababisha kundi la kigaidi la al-Qaeda la Osama bin Laden na makundi mengine kujiimarisha kwenye milima ya mpaka wa Afghanistan na Pakistan.
Karibu mataifa yote wanachama wa NATO yamekuwa yakisita kupeleka majeshi zaidi nchini Afghanistan, hivyo ongezeko hilo muhimu lazima litoke Marekani. Rais Barack Obama anatarajiwa kuidhinisha majeshi zaidi. Baadhi ya maafisa nchi za Magharibi katika mkutano huo wa Geneva walisema kuwa kuyaondoa mapema majeshi ya mataifa ya Magharibi yaliyoko nchini Afghanistan kutasababisha maafa. Nao baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema kuondoka haraka kwa majeshi hayo kunaweza kusababisha kundi la Taliban kuitwaa tena Kabul. Naye mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani, Zbigniew Brzezinski, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa ameupokea wito wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa wa kufanyika mkutano utakaoweka malengo mapya kwa Afghanistan kuchukua jukumu zima la kuhakikisha usalama wake na kuyaacha majeshi ya nchi za Magharibi kujiondoa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (REUTERS)
Mhariri: Miraji Othman