1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi lenye mafungamano na IS lafanya mashambulizi Misri

Admin.WagnerD30 Januari 2015

Idadi ya waliouawa katika mashambulizi yaliyowalenga wanajeshi na polisi katika rasi ya Sinai, Misri imeongezeka hadi 40 huku Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi akikatisha ziara nchini Ethiopia na kurejea nyumbani

https://p.dw.com/p/1ETJ4
Picha: imago/Xinhua

Kundi la Ansar Beit al Maqdis lenye mafungamano na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la dola la kiislamu IS limedai kuhusika katika mashambulizi hayo yaliyolenga kambi kadhaa za kijeshi na vituo vya polisi katika rasi ya Sinai kaskazini mwa Misri abako kumekumbwa na uasi.

Afisa wa afya wa Sinai Tareq Khater amesema miongoni mwa waliouawa ni maafisa wa usalama na raia na kuongeza kiasi ya watu wengine 36 wamepata majeraha.

Maafisa wa usalama wamesema makao makuu ya usalama ya jimbo hilo la Sinai, majengo ya idara ya ujasusi, kilabu cha wanajeshi, ofisi za gazeti moja na vituo vya ukaguzi vilishamabuliwa kwa makombora na mabomu ,hilo likiwa pigo kubwa la hivi karibuni dhidi ya vikosi vya usalama nchini Misri.

Asasi kadhaa za kiusalama zashambuliwa

Taarifa rasmi kutoka kwa ofisi ya Rais imesema al Sisi ameamua kukatisha ziara yake rasmi nchini Ethiopia ambako alihudhuria mkutano wa ufunguzi wa Umoja wa Afrika ili kurejea Cairo kutathmini hali ilivyo. Al Sisi alikuwa amepangiwa kuhutubia katika mkutano wa AU leo asubuhi.

Jeshi la Misri likishika doria katika rasi ya Sinai
Jeshi la Misri likishika doria katika rasi ya SinaiPicha: picture-alliance/dpa

Katika mtandao unaotumika na wanamgambo wa IS kutoa taarifa rasmi, kundi la Al Ansar limesema limefanya misuru ya mashambulizi kaskazini mwa Sinai kulipiza kisasi ukandamizaji wa serikali dhidi ya wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi ambapo mamia ya watu wameuawa, maelfu kufungwa jela na wengi kuhukumiwa kifo.

Marekani yalaani mashambulizi

Kundi hilo ambalo kwa sasa limebadilisha jina na kujiita dola la kiislamu la jimbo la Sinai limekuwa lilkifanya mashambulizi dhidi ya maafisa wa usalama. Mwezi Oktoba mwaka jana liliwauawa wanajeshi thelathini katika eneo hilo hilo la Sinai.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Jen Psaki amesema Marekani inalaani mashambulizi hayo na kuongeza nchi yake inasalia kujitolea kuisaidia serikali ya Misri kupambana na kitisho cha ugaidi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani Jen Psak
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani Jen PsakiPicha: AFP/Getty Images/N. Kamm

Msemaji wa jeshi la Misri Ahmed Samir amelilaumu kundi la udugu wa kiislamu kwa kupanga mashambulizi hayo.Taarifa fupi iliyowekwa katika ukurasa wake wa facebook imesema wanamgambo hao wamefanya mashambulizi hayo kutokana na mashambulizi yaliyofanikiwa dhidi yao yaliyofanywa na jeshi la Misri katika rasi ya Sinai na kuongeza maafisa wa usalama wanapambana na wanamgambo hao.

Uasi umeendelea katika rasi hiyo ya Sinai licha ya serikali kuanzisha hatua chungu nzima za kiuslama katika eneo hilo tangu mauaji ya wanajeshi mwaka jana.

Mamia ya maafisa wa usalama wameuawa na wanamgambo tangu kuondolewa madarakani kwa Mursi mnamo mwezi Julai mwaka 2013 na licha ya udugu wa kiislamu kukanusha kuhusika na makundi ya wanamgambo yanayofanya mashambulizi, serikali ya al Sisi imelishutumu kwa kuhusika na kulipiga marufuku kwa kuwa kundi la kigaidi.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/Reuters/Ap

Mhariri: Yusuf Saumu