1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

Kundi la Taliban limewauwa watu 8 katika uvamizi mjini Kabul

5 Januari 2023

Utawala wa Taliban umesema kwamba umewauwa watu wanane na kuwakamata wengine tisa wanaohusishwa na kundi linalojiita Dola la Kiislam- IS katika mfulizo wa uvamizi unaowalenga wanamgambo vinara wa IS mjini Kabul.

https://p.dw.com/p/4LlC7
Afghanistan Kabul | Explosion nahe Innenministerium: Taliban auf Militärfahrzeug
Picha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

Msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid, amesema uvamizi katika mji mkuu Kabul na mwingine kwenye jimbo la magharibi la Nimroz uliwalenga wanamgambo wa IS waliopanga mashambulizi ya hivi majuzi kwenye hoteli ya Longan mjini Kabul, ubalozi wa Pakistani na uwanja wa ndege wa kijeshi.

Mujahid amesema wapiganaji wanane wa IS, wakiwemo raia wa kigeni, wameuawa na wengine saba walikamatwa Kabul, wakati operesheni tofauti huko Nimroz ilifanikisha kukamatwa kwa wapiganaji wengine wawili wa IS.

Mwezi uliopita, utawala wa Taliban nchini Afghanistan ulitangaza kuwazuia wanawake kote nchini humo kujiunga na vyuo vikuu, katika wakati ambapo serikali hiyo ya msimamo mkali wa Kiislamu ikiendelea kukiuka haki na uhuru wa wanawake wa kupata elimu.

Agizo hilo liliibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya kimataifa iliyolaani vikali ukiukwaji huo.