Kundi la mataifa manne,Ujerumani,Brazil,India na Japan limewasilisha mapendekezo yao kuhusu kupanuliwa baraza la usalama la umoja wa mataifa
7 Julai 2005Kundi la nchi nne,linalozileta pamoja Ujerumani,Brazil,India na Japan limewasilisha mswaada wa azimio kuhusu namna ya kupanuliwa baraza la usalama la umoja wa mataifa.Kwa mujibu wa balozi wa Ujerumani katika Umoja wa mataifa bwana Gunter Pleuger,mataifa hayo manne yanashauri mjadala wa hadhara kuu ya umoja wa mataifa ufanyike jumatatu ijayo kabla ya mswaada huo kupigiwa kura.Mswaada huo unazungumzia juu ya kuongezwa idadi ya wanachama wa baraza la usalama toka 15 hivi sasa na kuwa wanachama 25,pakiwepo viti sita zaidi vya kudumu ambavyo wanachama wake hawatakua na haki ya kutumia kura ya turufu na wanachama wanne wengine ambao si wa kudumu.Kundi hilo la nchi nne,yaani Ujerumani,Brazil,India na Japan linashauri viti viwili vya kudumu kwa bara la Afrika.