1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kunakosekana Ulaya katika Umoja wa Ulaya

10 Septemba 2015

Wahariri wa magazeti ya leo(10.09.2015) Ujerumani wamejishughulisha zaidi na suala la wakimbizi na sera ya wakimbizi katika bara la Ulaya, mahakama yapiga marufuku mgomo wa marubani wa shirika la ndege la Lufthansa.

https://p.dw.com/p/1GUAh
Dänemark Polizei stoppt Zug mit Flüchtlingen
Polisi wa Denmark wakiwazuwia wakimbizi katika kituo cha treni mjini RodbyPicha: Reuters/Scanpix/J. Larsen

Gazeti la Landeszeitung , la mjini Lüneburg likizungumzia kuhusu hotuba ya rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya katika bunge la Ulaya mjini Strasburg , Jean-Claude Juncker linaandika:

Kunakosekana Ulaya katika Umoja huu. Na kunakosekana Umoja katika Ulaya hii. Jinsi suala hilo alivyoeleza Juncker , hakuna mtu ambaye anaweza kuuelezea msimamo wa Umoja wa Ulaya. Kwa mfano jinsi walivyouchukulia wito wake masaa kadhaa baadaye.

Maafisa wa Denmark wamebadilisha mtazamo wa wakimbizi waliokuwa wanaelekea nchini Sweden na kwa makusudi wamezuwia treni zote zinazotoka Ujerumani.

Sababu: Wale wasiotaka kuandikishwa kama wakimbizi nchini Denmark , watarejeshwa kule wanakotoka.

Kwa upande mwingine , Denmark inatambulika kwa sera zake kuhusu wakimbizi, zilizo katika msingi wa azimio la Dublin, licha ya kwamba sehemu kubwa imebadilishwa.

Na licha ya kwamba Juncker ametangaza sheria ya uhamiaji halali kuelekea bara la Ulaya mwaka 2016. Hili ni pigo kwa mkutano utakaofanyika wa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya.

Gazeti la Thüringischen Landeszeitung linaandika kuhusu wakimbizi waliozuiwa nchini Denmark: gazeti linasema.

Ulaya ambayo haina mipaka , imeanza kujenga kuta. Sio tu kiishara, lakini ni hali halisi kabisa. Umoja wa Ulaya ni lazima uchukue hatua na kupambana na hali ya uzalendo. Haiwezekani, kwamba Ujerumani , mataifa yanayopakana na bahari ya Mediterania na Hungary yaachiwe pekee mzigo wa wakimbizi. Iwapo Umoja wa Ulaya hautapambana na hali hii hivi sasa , nchi nyingine zitafuata mfano wa serikali ya siasa za wastani za kihafidhina mjini Copenhagen na kuanzisha udhibiti katika mipaka yao.

Hatua hiyo haitawazuwia wasafiri tu, lakini italeta matatizo makubwa. Huu ni mchezo wa kuwatuliza wafuasi wahafidhina wa mrengo wa kulia , kuliko suluhisho la kweli la matatizo hayo.

Nalo gazeti la Rheinischen Post likiandika kuhusu sera kuhusu wakimbizi katika bara la Ulaya linaandika:

Ni hali mpya kwa Ujerumani. Watu wamewalaki kwa shangwe wakimbizi, ambao maisha yao yalikuwa katika hatari na kuzikimbia nchi zao. Wamewasaidia kwa kuwapa misaada na kuwakumbatia , kiasi kwamba mashirika ya kutoa misaada hayakutambua kabisa, ni vipi yanaweza kuwatumia watu waliojitolea kutoa misaada. Hii inatia moyo sana , na tunaweza kujivunia kuhusu watu walivyokuwa tayari kutoa msaada.

Lakini wakati huo huo kuna hatari ya kuvurugika kwa kiasi kikubwa mshikamano katika Umoja wa Ulaya kuhusiana na ukarimu huu wa Ujerumani.

Nchi nyingi nyingine haziko tayari kufanya hivyo, zikitahadharisha kuhusu kuelemewa na mzigo huo.

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten , linazungumzia kuhusu mgomo wa marubani hapa Ujerumani.

Mgomo huo umesitishwa kutokana na amri ya mahakama, na kwa marubani hao si njia ya kutatua mgogoro huo na haitaleta hali nzuri katika majadiliano.

Marubani wameeleza kuwa wanataka mafao yao ya uzeeni wakati wakistaafu na mapema. Kwa hiyo marubani walikuwa wakigoma kwa lengo maalum, licha ya kuwa haikuwezekana kwa njia hii. Kwa kugoma huko hata hivyo mhariri anasema ni sawa na goli la kujifunga wenyewe kwa chama cha marubani.

Mwandishi:Sekione Kitojo

Mhariri:Yusuf Saumu