Uingereza na Marekani: Huenda ndege ya Urusi ililipuliwa
5 Novemba 2015Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, imeeleza kuwa baada ya kupokea taarifa zaidi, wanashuku huenda ndege hiyo ya Airbus chapa A321 ilianguka baada ya kifaa kulipuka ndani ya ndege. Kauli hiyo imetolewa wakati ambapo leo Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi anatarajiwa kukutana na Cameron mjini London, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu jeshi lilipomuondoa madarakani mtangulizi wake, Mohamed Mursi.
Akizungumza baada ya kukutana na kamati ya kudhibiti mizozo ya serikali ya Uingereza, inayoongozwa na Cameron, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Philip Hammond, amesema wakati uchunguzi unaendelea, hawawezi kusema moja kwa moja kwa uhakika ni kwa nini ndege hiyo iliangushwa.
Afisa wa Marekani amesema kuna uwezekano mkubwa bomu liliiripua ndege hiyo. Hapo jana, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuwa kisanduku cheusi ambacho kinarekodi mawasiliano ya ndege, kilirekodi sauti ambayo siyo ya kawaida wakati ndege hiyo ilivyokuwa ikiruka katika anga ya Sinai.
Imeripotiwa kuwa mwanga wa kimulimuli umenaswa na miale ya setilaiti ya jeshi la Marekani, ambayo wataalamu wa masuala ya anga wanasema hali hiyo inaashiria mambo mengi, ikiwemo kutegwa kwa bomu au kulipuka kwa ingini ya ndege baada ya kukumbwa na hitilafu.
Uingereza yasitisha safari zake za ndege
Uingereza imesitisha safari zake za ndege kwenda Sharm el-Sheikh, kama tahadhari, hadi tathmini ya kiusalama itakapokamilika. Mabaki ya ndege hiyo na kisanduku cheusi cha kurekodia mawasiliano ya ndege, bado yanafanyiwa uchunguzi.
Hata hivyo, ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza, imesema Al-sisi na Cameron wamekubaliana kuhusu haja ya kuimarisha usalama kwenye uwanja wa ndege wa Sharm el-Sheikh na wataalamu wa anga wa Uingereza wamepelekwa kwenye mji huo kutathmini hali ya usalama.
Hayo yanajiri wakati ambapo kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu-IS likiendelea kusisitiza kuhusika na ajali hiyo, likisema limefanya hivyo kutokana na hatua ya Urusi kuivamia kijeshi Syria kupambana na kundi hilo.
Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na Urusi na Misri. Wataalamu wa masuala ya anga wa Misri wanaovichunguza visanduku viwili vya kurekodia mawasiliano ya ndege, wamesema wamechukua data kutoka kwenye moja ya visanduku hivyo kwa uchunguzi zaidi. Wamesema kisanduku kingine kimeharibiwa, hivyo kazi ya ziada inahitajika kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Ndege hiyo ilianguka dakika chache baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa mji wa kitalii wa Sharm el-Sheikh, ikielekea St. Petersburg, na kuwaua abiria wote 224 waliokuwemo ndani.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE, DPAE
Mhariri: Daniel Gakuba