Kumbukumbu ya miaka 65 ya shambulio la Hiroshima.
6 Agosti 2010Shambulio hilo lililofanywa na Marekani, lilikuwa la kwanza kutumia silaha za nyuklia.
Ni kengele ya amani ya Hiroshima ambayo imelia leo saa mbili na robo asubuhi katika mji wa Hiroshima ikiwa ni muda kamili miaka 65 iliyopita, ambapo Marekani ilidondosha mabomu ya atomiki katika mji huo ulioko magharibi mwa Japan na kuua maelfu ya watu kwa sekunde moja na wengine maelfu kwa maelfu kufa taratibu kwa miongo kadhaa iliyopita tangu kutokea shambulio hilo mwaka 1945.
Kumbukumbu hiyo ya miaka 65 toka kufanyika kwa shambulio hilo imefanyika katika mnara wa kumbukumbu karibu na eneo la ground zero, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali ndani na nje ya nchi hiyo, akiwemo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-Moon, ambapo pia kwa mara ya kwanza Marekani iliwakilishwa na balizo wake, John Ross.
Katika eneo hilo la kumbukumbu watu walikaa kimya dadika moja kuwaombea marehemu.
Ban ataka ukomeshaji wa nyuklia:Akizungumza katika kambukumbu hiyo mjini Hiroshima, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, BanKi-moon, ambaye amekuwa kiongozi wa kwanza wa umoja huo katika nafasi hiyo kuhudhuria tukio hilo la mwaka, amesema kwa pamoja tunaelekea katika njia ya kukomesha utumiaji wa silaha za nyuklia kutoka katika eneo moja kuelekea dunia nzima.
Ban ki-Moon ametolea mfano wake binafsi kutokana na funzo alilolipata wakati wa vita vya Korea vya mwaka 1950 hadi 53, hali iliyomfanya kuanza kutafuta amani.
Aidha katibu mkuu wa Umoja wa mataifa ameitaka pia jumuiya ya kimataifa ihakikishe mkataba unaopiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia unaanza kufanya kazi mwaka 2012, pamoja na kufanyika mikutano ya mara kwa mara ya baraza la usalama la umoja huo kutathmini utekelezaji wake, ikiwa ni kufuatia ule wa mwaka jana 2009.
Kwa upande wake, meya wa mji wa Hiroshima, Tadatoshi Akiba, ameitaka serikali ya Japan kupitisha sheria juu ya mambo matatu ya msingi dhidi ya silaha za kinyuklia, ambayo ni utengenezaji, umilikaji na utoaji wa silaha za aina hiyo.
Katika hatua nyingine, meya huyo wa mji wa Hiroshima ameupongeza uamuzi wa Marekani kumtuma balozi John Roos wa nchi hiyo katika kumbukumbu hiyo ya miaka 65, ikiwa ni ya kwanza kwa Marekani kutuma mwakilishi.
Aidha hatua hiyo ya Marekani kushiriki katika tukio hilo kwa mara ya kwanza imeelezwa kuonesha matumaini ya kuimarisha juhudi za kupunguza silaha hizo za nyuklia.
Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,ap)
Mhariri: Miraji Othman