kumbukumbu ya miaka 60 ya ukombozi wa kambi ya Auschwitz
24 Januari 2005Alhamisi wiki hii tarehe 27 Januari itatimia miaka 60 tokea kukombolewa kambi ya Auschwitz na majeshi shirika yalioshinda vita vya pili vya dunia Aidha tarehe hiyo ni kumbukumbu ya maovu yaliofanywa na utawala wa Hitler kuanzia Juni 1940 hadi Januari 1945.
Ulikua ni wakati wa mchana pale wanajeshi wa jeshi jekundu la iliokua Urusi yazamani, walipoingia katika kambi hiyo ya Auschwitz na kuiteka tarehe 27 Januari 1945. Wanajeshi wa utawala wa wanazi wa Hitler walikua tayari wameshaihama kambi hiyo pamoja na silaha zao nzito. Wanajeshi hao wa Urusi wakawakuta wale mia kadhaa waliosalimika kutokana na idadi ya maelfu ya waliouwawa ,wakiwa katika hali ya uchovu na waliodhoofika kimwili.
Katika ghala za kambi hiyo kukakutikana nguo za wanaume , wanawake, na watoto na viatu , pamoja na karibu tani saba za nyewele za binaadamu zilizofungwa kwa uangalifu kwenye mifuko ya karatasi. Ulikua ni ushahidi wa mauaji ya halaiki katika kiwango ambacho dunia haikupata kukishuhudia.
Tangu Juni 1940 walikua wafungwa wakipelekwa katika kambi hiyo karibu na mji wa Krakau nchini Poland, kutokana na ubaguzi chini ya misingi ya kisiasa , kidini na wa kijamii –wimbi lililoikumba karibu ulaya nzima ,na yote yakawa ni dhidi ya Wayahudi. Zaidi ya Wayahudi milioni moja, wanaume, wanawake na watoto waliuwawa kambini humo.Auschwitz kambi kubwa ya mateso ikiwa ni janga la moto duniani.
Ama yaliotokea yametoa funzo. Nalo ni kwamba hisia za utaifa na uzalendo, mshikamano na waovu, chuki dhidi ya Wayahudi, ni mambo ambayo lazima yawe mwiko na yasiyopaswa kushuhudiwa tena kuanzia ulaya ya kati hadi ya Mashariki.-
Ushahidi unaokutikana katika kambi ya Auschwitz kuanzia makaburi ya wahanga, vyumba vya gesi vya mauaji na mahandaki , vyote ni funzo na miaka hii 60 ya ukombozi wa kambi hiyo , pia ni kumbukumbu ya yaliotokea.
Katika kujifunza huko kuna mchango pia unaohitajika. Kuepusha janga kama hilo. Tayari kupigwa hatua kwai kesi zimefanyika na wahusika kuhukumiwa, vitabu vimeandikwa na filamu za kihistoria juu ya matukio hayo kutengenezwa lakini kuna kubwa zaidi,-wakati wengi walionusurika sasa wameshafariki, na kuna uwezekano miongoni mwa walio hai hadi sasa pengine hawatoshuhudia kumbukumbu ya miaka 70, ni muhimu kuungana nao katika kumbukumbu hii ya miaka 60.
Pana haja kubwa hivi sasa baada ya kun´golewa ufashisti, na baadae udikteta wa Kisovieti, ya watu kukaa pamoja na kutafakari pamoja na mataifa machanga ya Baltic, Jamhuri ya Cheki, Hungary na Rumania na pia Ukraine na kutafakari.
Mataifa haya yanahitaji kujongeleana na kuzungumza, pamoja na kusaidiwa ili yaweze kupiga hatua.
Ni muhimu mno-miaka 60 baada ya kumalizika kwa mauaji ya halaiki yaliofanywa barani ulaya na utawala wa wanazi katika Ujerumani,na kufunguliwa ukurasa wa maadili mapya ya kitamaduni katika bara hili
Ni dhahiri kuwa kwa pamoja, ulaya inaweza kufungua ukurasa mpya na ni jambo la dharura. Na hapa kuna suala lilo wazi, vipi kielimishwe kizazi kijacho juu ya mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi ?
Chini ya mtazamo huu, kambi ya mateso ya Auschwitz, panasalia kuwa mahala na alama muhimu ya kutafakari na kujifunza. Sambamba na hayo mwaka huu 2005 hauna budi kuwa ni mwaka wa kutafakari, wakati wa kumbukumbu hii ya miaka sitini ya tangu kukombolewa kwa kambi ya mateso ya Auschwitz