1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kukosekana kwa uhuru wa Vyombo vya habari nchini Zimbabwe, waandishi matatani.

Scholastica Mazula3 Juni 2008

Waandishi wa habari nchini Zimbabwe wanakabiliwa na matatizo kadhaa katika utoaji habari kitendo kinahowalazimisha kutumia vyombo vya habari vya kimataifa ili kueleza hali halisi iliyoko nchini mwao.

https://p.dw.com/p/EC5q
Itai Mushekwe,-Kushoto, mwandishi wa habari za Kisiasa kutoka Zimbabwe, Rose Kimotho, Mkurugenzi wa Radio Kameme nchini Kenya na Christopher Springate, mwandishi wa habari wa DW.TV nchini Ujerumani, wakiwa katika Kongamano la Kimataifa la waandishi wa Habari.Picha: DW

Hii ni kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na waandishi wa habari wa Zimbabwe katika Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya habari linalofanyika Mjini Bonn, Ujerumani.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili katika kongamano hilo mwandishi wa habari za kisiasa kutoka nchini Zimbabwe, Itai Mushekwe, ameelezea kusikitishwa kwake na hali ya Zimbabwe na kusema kuwa hali hii inachangiwa na Chama tawala kuendelea kung'ang'ania madarakani.

Itai Mushekwe, anasema nchini Zimbabwe hakuna uhuru wa vyombo vya habari kwa sababu rais wa nchi hiyo Robert Mugabe, amevibana vyombo vya habari vingi na kubakisha vichache ambavyo vinaandika habari zake kwa matakwa ya Serikali.

Anasema hali ya Zimbabwe kwa sasa ni mbaya sana, hali ya kiuchumi na Kisiasa inazidisha hofu miongoni mwa wananchi na kwa upande wa waandishi wa habari ni vigumu sana kufanya kazi ndani ya Zimbabwe kwa sababu ya mazingira yalivyo, wandishi wanakamatwa, wanateswa na wengine kwa bahati mbaya wanapoteza maisha yao.

Kutokana na kwamba wanahabari wa Kimataifa hawawezi kufanya kazi za uandishi kwa sababu ya mazingira ya hatari yaliyopo na Rais Mugabe kutowaruhusu, Waandishi hao wa Kimataifa huwatumia waandishi wa Zimbabwe ili kupata hali halisi nchini humo.

Hata hivyo anasema jambo linalowasikitisha kwa bahati mbaya hata baadhi ya waandishi wa Kimataifa huziandika habari hizo kwa matashi ya Vituo vyao na maeneo wanayofanyia kazi.

Lakini mbali na matatizo wanayokabiliana nayo kama waandishi wa habari nchini Zimbabwe wanafanya nini ili kutoa taarifa zao na hali ya nchi hiyo.

Mushekwe anafafanua kuwa kama wandishi wa habari wa Zimbabwe walioko ndani na wanaofanya kazi nje ya nchi wanajaribu kukusanya ripoti za mambo yanayotokea nchini Zimbabwe na kujaribu kuziandika kisha kuzituma kwenye vyombo vya habari vya Kimataifa, wakiamini kuwa hili linaweza kusaidia kufanya matatizo hayo kuwa ya Kimataifa.

Waadishi wa habari wamekuwa wakikumbana na matatizo mbalimbali katika kazi yao, kutokana na kutaka kuandika ukweli kuhusu sera na matatizo ya nchi ama Serikali husika.

Mwandishi huyo kutoka Zimbabwe anasema kwa bahati mbaya Serikali hususani katika nchi zenye migogoro kama Zimbabwe, mgogoro wa Kenya, Sudan na maeneo mengine zimekuwa hazitaki kukosolewa hata kuambiwa ukweli na Vyombo vya habari na hivyo kujikuta zikijaribu kuvibanavyombo hivyo ama kuwaua waandishi wa habari ili kuficha uovu unaofanyika ndani ya nchi husika.

Kwa upande wake, Mushekwe anashauri kuwa Waandishi wa habari wanapaswa kukaa pamoja na kufanya kazi kama familia moja, kwa sababu kama kutakuwepo na migogoro Zimbabwe au Darfur na maeneo mengine ni waandishi wa habari ndiyo wanakuwa katika wakati mgumu sana kwa hivyo wanahitaji kusaidiana.

Kongamano hilo la siku tatu la waandishi wa habari lililotayarishwa na Deutsche welle, limewashirikisha waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali zikiwemo, Tanzania, Kenya, Sudani, Zimbabwe, Sierra Lione, Ghana na nyingine za ulaya na linatarajiwa kumalizika kesho Juni nne.