Kukabiliwa kwa mashitaka ya Uhaini kwa Katibu Mkuu wa chama cha MDC nchini Zimbabwe, Tendai Biti, huwenda kukamfanya akabiliwe na adhabu ya kifo.
13 Juni 2008Hii inafuatia kukamatwa kwake jana, ikiwa ni dakika chache tu baada ya kurejea nchini humo kwa ajili ya kufanya kampeni za kuelekea katikaUchaguzi Mkuu wa Urais utakaofanyika Juni ishirini na saba.
Wakati huohuo rais Robert Mugabe ameonya kwamba Vijana wake wanaomuunga mkono wako tayari kushika silaha kuliko kukiona chama cha upinzani kikiingia madarakani na kwamba atawatumia zaidi wakongwe wa vita, Maveterani.
Mbali na kukamatwa kwa Katibu Mkuu wa chama cha MDC, Tendai Biti, polisi pia jana walimkamata mara mbili kiongozi wachama hicho na mgombea wa Urais, Morgan Tsvangirai katika kituo cha kati nchini Zimbabwe naa kumshikilia kwa masaa mawilli ya awali na pia kwa kiasi cha masaa manne baadaye baada ya kumwachia huru.
Tendai Biti, huwenda akakabiliwa na adhabu ya kifo endapo atapatikana na makosa ya uhaini, Mashitaka ambayo anakabiliwa nayo, nikutaka kujaribu kukifanya chama cha MDC,kishinde katika awamu ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika miezi mitatu iliyopita.
Biti, mpinzani mkubwa wa Rais Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka themanini na nne, na ambaye amekuwa akimshutumu rais huyo kwa kujaribu kutaka kuchukua madaraka kwa gharama yoyote, alikamatwa jana hata kabla hajafika katika sehemu ya ukaguzi wa hati za kusafiria kwenye uwanja wa ndege wa mjini Harare.
Katika kipindi cha wiki mbili sasa, Tsvangirai, amekuwa akisisitiza kumshinda rais Mugabe katika duru ya pili ya uchaguzi baada ya matokeo ya awamu ya kwanza kuonekana wote kuwa hakuna aliyemzidi mwingine.
Hata hivyo, katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa, uliofanyika mjini NewYork, Marekani, Mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja huo, John Holmes, alionya kwamba hali ya njaa itakayoikabili Zimbabwe, ni kiasi cha robo tu, ya watu wote watakaopata chakula nchini humo.
Holmes, ambaye anashughulikia masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, amesema hali ya ukosefu wa chakula nchini humo ni mbaya sana, ambayo endapo hazitachukuliwa hatua za haraka, watu wengi wataweza kukabiliwa na ukosefu wa chakula.
Amewaambia waandishi wa habari kwamba, kadri siku zinavyokwenda, Wazimbabwe wanahitaji msaada, kutokana na kushuka kwa uchumi wa nchi hiyo na kuharibiwa kwa huduma za kijamii.
Akiwa ameongoza kwa miaka ishirini na nane nchini Zimbabwe, Rais Robert Mugabe, anakabiliwa na changamoto kubwa ya uchaguzi, kutoka kwa Morgan Tsvangirai, mgombea pekee aliyejitupa katika kinyang'anyilo cha duru ya pili ya urais, baada ya ile ya kwanza aliyodai kuwa ameshinda kwa zaidi ya asilimia hamsini ya kura.
Hadi sasa, Tsvangirai, ameshakamatwa na polisi katika matukio manne katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita.
Chama cha MDC, kimesema mpaka sasa kiasi cha wafuasi wake sitini wameshauawa tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi.
Serikali ya Rais Mugabe, imewazuia waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi za Magharibi, lakini imewaruhusu waangalizi wa Afrika katika duru hii ya pili, wakiwemo kutoka nchi kumi na nne wanachama wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika,SDC, ambao kwa mujibu wa SDC, tayari wameshaanza kupelekwa nchini humo.