Kujiuzulu Oezil timu ya taifa kwazua zogo Ujerumani
23 Julai 2018Matokeo yaliyotarajiwa kuhusiana na suala la Mesut Oezil yamesababisha majibu ambayo hayakutarajiwa. Hakuna mtu katika masimulizi haya ya kusikitisha amejitokeza kuwa mshindi katika sakata hili.
Mesut Oezil alijiuzulu kutoka katika timu ya taifa ya Ujerumani Die Mannschaft kwa kuwashambulia vikali , wafadhili, vyombo vya habari, chama cha kandanda nchini Ujerumani DFB na hususan rais wa shirikisho hilo, lakini ni vigumu kuona kila upande kuwa ni kitu kingine mbali na washindwa katika suala hili la kusikitisha.
Gazeti la Sueddeutsche Zeitung limeueleza uamuzi wa mchezaji huyo kuwa ni " kipigo kamili cha majira ya joto" wakati mtaalamu maarufu wa soka la Ujerumani Raphael Honingstein aliandika katika ESPN kuhusiana na kujiuzulu Oezil kutoka katika timu ya taifa kuwa " ni hali mbaya kuliko kushindwa kokote katika kombe la dunia."
Oezil, katika kuvunja ukimya wake jana Jumapili kuhusiana na picha zenye utata zilizopigwa akiwa pamoja na rais wa Uturuki Recep Erdogan kabla ya fainali za kombe la dunia nchini Urusi, hakuonesha kujutia kitendo hicho na ameonesha kukasirishwa mno.
Hali ya kisiasa
"Natambua kwamba picha hizo zimesababisha maelezo mengi katika vyombo vya habari vya Ujerumani, na baadhi ya watu huenda wakanishutumu mimi kwa udanganyifu ama kuwa muongo, picha hizo hazina lengo la kisiasa," amesema Oezil, mzaliwa wa Gelsenkirchen nchini Ujerumani akiwa na asili ya Uturuki.
Iwapo hilo ni kweli, inaonekana kwamba Oezil hajitambui kwa kufikiri kwamba hakutakuwa na uhusiano utakaohusishwa na picha hizo zilizopigwa wiki chache kabla ya Erdogan kuwania kuchaguliwa tena, kutokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini Uturuki.
Hata hivyo kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemshukuru Mesut Oezil kwa mchango wake katika timu ya taifa , Die Manschaft, amesema msemaji wa serikali ya Ujerumani leo. "Kansela anamthamini Mesut Oezil kwa hali ya juu kabisa. Mesut Oezil ni mchezaji kandanda mzuri sana ambaye ameifanyia mengi timu ya taifa," msemaji wa kansela amesema.
"Mesut amefanya sasa uamuzi wa kujitoa kutoka timu hiyo na ni lazima uamuzi wake uheshimiwe," alimaliza msemaji huyo wa kansela. Mesut Oezil leo ameweka picha yake kwa mara ya kwanza tangu tafarani hii kuzuka hapo jana akiwa na jezi za klabu yake ya Arsenal ya mjini London, akionesha furaha kurejea kwa amani katika kusakata kandanda tena bila ya kuwa na mzigo wa timu ya taifa ya Ujerumani.
Wakati huo huo kamati ya utendaji ya shirikisho la kandanda nchini Ujerumani DFB iliyoketi leo na kujadili suala hilo imetupilia mbali madai ya ubaguzi yaliyotolewa na Mesut Oezil dhidi ya rais wa shirikisho la DFB Reinhard Grindel katika barua yenye hasira ya kujiuzulu. "Tunapuuzia dhana kwamba DFB inahusika na ubaguzi," imeeleza taarifa.
Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Idd Ssessanga