Kuishi na ulemavu wa ngozi nchini Kenya, nini cha tofauti?
Kuishi na ulemavu wa ngozi kunaweza kuwa hatari katika nchi nyingine za Afrika. Nchini Kenya, unyanyapaa upo, lakini kuna unafuu. Kwenye albamu hii, vijana watatu wanasimulia kuhusu kuishi na ulemavu huo jijini Nairobi.
Elimu ni ufunguo- Kutana na Daniel.
Watu wenye ulemavu wa ngozi mara nyingi hawapati elimu nzuri bora kwa sababu ya unyanyapaa. Kwa hiyo sisi [katika taasisi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ya Kenya] tulikuja na mipango ya kuwawezesha kuanza biashara zao wenyewe na kujitegemea. Kwa njia hiyo wanaweza kutunza familia zao na kuwa na uwezo wa kujitegemea wenyewe, anasema Daniel Shisia, msemaji wa taasisi hiyo.
'Mzungu Reloaded' - Kutana na Whycliffe.
Kibera ni eneo la makazi holela jijini Nairobi. Watu milioni moja wanaishi hapa. Katika moja ya mitaa yenye shughuli nyingi, kati ya duka la viatu na kioski, kuna duka linaloitwa "Mzungu Reloaded." "Mzungu" ikimaanisha "mtu mweupe". Whycliffe anamiliki duka, lakini sio "mzungu" halisi, ila ana ulemavu wa ngozi. "Niliamua kuliita 'Mzungu Reloaded' kwa sababu mimi ni kama mzungu," alisema Whycliffe.
Jina lake kama alama ya biashara.
Barani Afrika watu wenye ulemavu wa ngozi ni wengi zaidi kuliko mahali popote duniani. Mbali na ubaguzi, wanakabiliana na matatizo ya ngozi kutokana na jua kali na uoni hafifu. Kwa hiyo Whycliffe huvaa kofia na miwani. Aliamua kutumia rangi yake ya ngozi "nyeupe" kama alama ya biashara yake.
Kukubalika zaidi na uwezeshaji.
"Kila mahali nitakapokwenda, wananiita 'mzungu' 'mzungu'. Nilidhani, 'ni alama gani ya biashara ambayo ninaweza kutumia kwa biashara yangu?' Ndiyo maana nimechagua jina hili. Watu wengi hawatumii jina hili kwa nia mbaya, ni njia ya kunikubali, sio hatari. " Whycliffe ni mrithi wa mpango wa uwezeshaji wa kiuchumi, mradi wa taasisi ya wenye ulemavu wa ngozi la Kenya, inayofanya utetezi na utambuzi.
Kupatiwa fursa .
Daniel ni msemaji wa taasisi ya wenye ulemavu wa ngozi ya Kenya. Anaelezea umuhimu wa watu wenye ualbino kuwa na kazi za kawaida na biashara ili kujihisi kuwa sehemu ya jamii. "Nchini Tanzania na nchi nyingine za jirani, watu wamekuwa wakiuawa, lakini hapa hawauwawi, lakini wanabaguliwa kwenye ajira. Tunajihisi kama hatupewi fursa hii, hatupewi nafasi hiyo."
Whycliffe anaweza kuisaidia familia yake, akiwa na biashara yake.
"Niliona vigumu kupata kazi .. Watu wengine hawakunikubali, walidhani siwezi kufanya kazi. Nilikwenda sehemu nyingi lakini sikupata kitu. Biashara hii imenisaidia kutunza familia yangu na kununua mkate. Nimeweza kununua nyumba Kibera kwa mikopo. ."
Ufahamu na kukubalika kunazidi kuimarika- Kutana na Francis.
Francis anaishi Makadara, mashariki mwa Nairobi. Pia anamiliki duka ndogo akiuza mayai, mikate na sukari. Aligundua kwamba bahati yake ilianza kubadilika wakati alipoanza kujikubali mwenyewe. Hutoa pia huduma ya kuhamisha fedha na biashara yake inakua. "Wateja wangu wananikubali, wanakuja na kuniachia fedha zao." Hii inamaanisha kukubalika kwa Francis kuna maana kubwa kwake.
Nchini Kenya tuko salama.
Francis anasema hajawahi kuhisi kubaguliwa akiwa Kenya. Lakini Daniel anakumbuka kwamba sio zamani sana, alipokuwa mtoto hofu ambayo aliweza kuwa nayo anapokua katika nchi nyingine kwa kuwa na ulemavu huo labda ya kuuawa bado ilikuwa imeenea. Whycliffe, Francis na Daniel wanaonyesha kwamba kuishi na ulemavu huo hakumaanishi kuwa maisha yao ni tofauti kabisa na wengine.
Picture gallery: Eva de Vries, Nairobi, Kenya