kufuatia maadhimisho ya Juma Kuu la Kwaresma Vatican yapinga shutuma za Osama Bin Laden dhidi ya Papa Benedikto wa kumi na sita.
21 Machi 2008kufuatia maadhimisho hayo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Benedikto wa Kumi na Sita amesema hakuna binadamu atakayeweza kuwa mkamiliffu pasipo kujitoa maisha yake kwa Mungu.
Baba Mtakatifu ametoa ujumbe huo jana katika maadhimisho ya siku ya Alhamisi kuu katika mahubiri yakee kwenye Ibada ya Misa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Amefafanua kwamba anapozungumzia kujitoa, ni kile kitendo cha kujitoa pasipo kujibakiza kumfuata Mungu mmoja nakuwa na fikra kwamba Binaadamu kwa kawaida hawezi kuwa mkamilifu isipokuwa kwa njia ya Uhuru huo usiokuwa na pingamizi.
Ibada maalumu ya kubariki mafuta ya Krisma iliadhimishwa jana na kuongozwa na Maaskofu wa kila Jimbo Katoliki duniani kote.
Katika Ibada hiyo Maaskofu walibariki Mafuta ya Krisma ambayo yatatumika katika kipindi cha mwaka huu wote hadi mwaka 2009 kwa ajili ya Ubatizo na Sakramenti nyingine Takatifu na siku hiyo Mapadri wote hurudia ahadi zao walizozitoa siku ya Upadrisho.
Aidha jana Vatican ilikanusha shutuma dhidi yake ambazo zimekuwa zikitolewa na kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Osama bin Laden kwamba Papa amekuwa akishiriki moja kwa moja kwa kile wanachokiita Vita vitakatifu dhidi ya Uislamu kwa kusambaza Katuni zinazomuonyesha Mtume Muhammed.
Jana Osama bin Laden alitoa ujumbe wa kuzionya nchi za Ulaya juu ya Katuni hizo na kudai kwamba machapisho yao yalitengenezwa ikiwa ni sehemu ya kazi iliyofanya na kundi linapigana Vita Vitakatifu ambavyo Baba Mtakatifu anashutumiwa kushiriki kwa kiwango kikubwa.
Kwa mujibu wa Shirika moja la habari nchini humo -ANSA, Waziri wa Ulinzi wa ndani wa Italia ambaye ndiye mlinzi Mkuu wa Papa Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuutathimini kwa kina ujumbe huo wakati wa Mkutano utakaofanyika leo katika baraza lake la kupinga Ugaidi.
Lakini msemaji wa Vatican FEDERICO LOMBARD, amesema kitisho hicho hakiwezi kuvuruga taratibu za kiuchungaji za Kiongozi huyo wa madhehebu ya Kikatoliki duniani na zaidi katika kipindi hiki cha Pasaka ambako ulinzi utaimarishwa zaidi.
Leo Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita ataongoza njia ya Msalaba na ataubeba katika vituo vitatu kati ya vituo kumi na nne vya njia ya msalaba.
Papa Benedikto wa Kumi na Sita, aliyeteuliwa mwaka 2005,kuwaongoza waamini wa Kanisa Katoliki Duniani baada ya kifo cha mtangulizi wake Papa Yohane Paulo wa Pili, atabeba msalaba katika kituo cha kwanza na cha mwisho.
Ibada ya Misa ya Pasaka itaadhimishwa jumapili katika Viwanja vya Mtakatifu Petro mjini Vatican ambapo waamini watasomewa ujumbe wa pasaka uliotolewa na papa unaosema "Kwa watu wote katika miji na kwa Ulimwengu mzima".