1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufanyika kwa duru ya pili ya Uchaguzi nchini Afghanistan

20 Oktoba 2009

<p>Rais Hamid Karzai wa Afghanistan, huenda leo akatangaza msimamo wake, kama yuko tayari kwa duru ya pili ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/KAst
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akabiliwa na shinikizo la kimataifa kuhusu kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguziPicha: AP

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kimataifa, huenda leo akatangaza msimamo wake, kama yuko tayari kwa duru ya pili ya uchaguzi kufuatia matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais nchini humo kukumbwa na utata, na baada ya Tume ya kusikiliza malalamiko ya uchaguzi nchini humo, kuamuru kwamba, kura kutoka vituo 210 vya uchaguzi nchini Afghanistan zitangazwe kuwa hazifai na batili.

Uchaguzi Mkuu wa Rais nchini Afghanistan uliofanyika Agosti 20, ambao umedaiwa kukumbwa na udanganyifu, umechochea wasiwasi kati ya Rais Karzai na serikali za nchi za magharibi ambazo majeshi yao, yanapigana na wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan.

Akizungumza mara tu baada ya Tume hiyo ya kusikiliza malalamiko ya uchaguzi kutangaza ripoti yake, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema anatarajia leo kusikia chochote kutoka kwa Rais Karzai na kuweka matumaini ya kupatikana kwa ufumbuzi wa haraka.

Hillary Clinton 2009
Bibi Hillary Clinton aweka matumaini kwa Rais Karzai kupata ufumbuzi wa harakaPicha: AP

Katika mikutano ya faragha aliyoifanya wiki hii, ikiwemo na ule alioufanya na Seneta John Kerry wa Marekani, Rais Karzai alionesha kuwa tayari kushiriki katika raundi ya pili ya uchaguzi na mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah, lakini hata hivyo hakutoa ratiba kamili.

Hata hivyo wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba Rais Karzai, ambaye anatokea katika jamii ya Pashtun, iliyo kubwa nchini Afghanistan, anaweza akashinda katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi.

Lakini maofisa wanatahadharisha kwamba Rais Karzai anaweza kubadili mawazo yake, hali itakayosababisha pengine mabishano makali ya kisiasa.

Akizungumza leo, mjini Kabul msemaji wa Bwana Waheed Omar amesema Rais Karzai atakubali matokeo ya mwisho yatakayotolewa na tume ya uchaguzi.

Amesema wanasubiri matokeo yatangazwe na Tume huru ya uchaguzi na mara itakapotangaza watalazimika kukubali.

Taasisi ya Kimataifa inayoshughulika na masuala ya Demokrasia pamoja na taasisi ya Amani yenye makao yake mjini Washington, zimesema ripoti iliyotolewa na Tume ya kusikiliza malalamiko ya uchaguzi imeonesha kwamba Rais Karzai amepata asilimia 48.3 ya kura zilizopigwa, wakati jumla ya asilimia alizopata mpinzani wake Abdullah Abdullah imeongezeka kufika 31 kutoka ya awali ya asilimia 28.

Abdullah Abdullah
Abdullah Abdullah, mpinzani mkuu wa Rais Hamid KarzaiPicha: DW

Mwanadiplomasia mmoja wa nchi za magharibi mjini Kabul ambaye hakutajwa jina lake anaonesha uelekeo zaidi wa kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi, ambapo Umoja wa Mataifa nao umejiandaa kwa hali hiyo kama anavyoelezea msemaji wa Umoja huo mjini Kabul, Aleem Seddique.

Maandalizi tayari yanaendelea vizuri kwa ajili ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi, vifaa vyote vya kupigia kura ambavyo vinahitajika kuendesha duru ya pili ya uchaguzi kwa sasa vipo hapa nchini, usambazaji utaanza kufanywa wiki ijayo iwapo Tume huru ya Uchaguzi itatangaza haja ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi...''

Madai hayo ya kufanyika kwa udanganyifu wakati wa uchaguzi, yamekuwa yakitatiza dhamira ya Rais Barack Obama wa Marekani juu ya uamuzi wake wa kupeleka maelfu ya wanajeshi, katika juhudi za kumaliza ghasia nchini humo.

Naye Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates, akizungumza na Waandishi wa habari, wakati akiwa njiani kuelekea Tokyo Japan kwa ziara ya siku mbili, amesema nchi yake haiwezi kusubiri mpaka pale matatizo yanayoikabili serikali ya Afghanistan kupatiwa ufumbuzi, kabla ya kufanya uamuzi juu ya vikosi hivyo vya jeshi.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri:Hamidou Oummilkheir