Krismasi bila shamrashamra
24 Desemba 2015Kawaida, wakati wa msimu wa siku kuu ya Krismasi, ukipita mitaani utaona miti ya Krismasi ikimeremeta kwelikweli, huku kukiwa na mapambo ya kila aina. Kuna wale ambao huhudhuria ibada za mkesha wa Krismasi huku wengine wakijumuika na marafiki katika kumbi za burudani. Lakini mwaka huu mambo yatakuwa tofauti kabisa katika nchi za Somalia, Tajikistan, na Brunei, ambako viongozi katika kila nchi wametangaza hatua kali za kupiga marufuku sherehe za Krismasi na mapambo kwa sababu mbalimbali.
Somalia
Nchini somalia, serikali imepiga marufuku sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ikisema sherehe hizo hazihusiani kwa vyovyote vile na Uislamu. Mkurugenzi wa wizara ya dini ya Somalia, Sheikh Mohamed Kheyrow amesema wizara yake imetuma barua kwa polisi, ofisi ya ujasusi ya kitaifa pamoja na maafisa wengine katika mji mkuu Mogadishu ikiwataka kuzuia sherehe za Krismasi.Kando na kuwa na idadi kubwa ya Waislamu, Somalia ni mwenyeji wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, wakiwemo wa nchi zilizo na Wakristo wengi za Burundi, Uganda na Kenya. Msemaji wa meya wa Mogadishu, Abdifatah Halane, amesema sherehe hizo zimefutwa kwa sababu mbili. Kwanza, Wasomali wote ni waislamu na hakuna jamii ya Wakristo nchini humo. Pili, sherehe za Krismasi huenda zikachochea mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa al-Shabaab.
Brunei
Nchini Brunei, Krismasi imepigwa marufuku kabisa, serikali ikisema sikukuu hiyo ni kinyume na mafundisho ya utamaduni wa Kiislamu wa taifa hilo dogo tajiri la Asia ya Mbali. Atakayekiuka marufuku hiyo anaweza kufungwa jela miaka mitano. Ijapokuwa Wakristo wako huru kusherehekea wameambiwa kutofanya hivyo kwa kupindukia na wazi wazi.
Wenye maduka wameonywa kuondoa kabisa mapambo huku maafisa wakifanya msako katika mji mkuu, Darusalaam. Hoteli kubwa kubwa maarufu kwa watalii wa nchi za magharibi zilizokuwa zikimeremeta sasa hazina mapambo yoyote.
Nchini Tajikistan, miti ya Krismasi imepigwa marufuku katika shule. Amri ya wizara ya elimu imepiga marufuku pia “matumizi ya fataki, mapochopocho ya vyakula vya sikukuu, kupeana zawadi na kuchangisha fedha“ kwa ajili ya sherehe za Mwaka Mpya.
Hatua hizi zinachukuliwa kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha vikwazo dhidi sherehe za sikukuu za kimagharibi kwa jumla. Mwaka jana na juzi, watu waliovalia mavazi ya kutisha, maarufu kama mazombi kwenye sherehe za Halloween, waliripotiwa kuwekwa kizuizini na polisi nchini Tajikistan
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohamed Khelef