Korea ya kaskazini yazidisha vitisho vya vita
9 Aprili 2013"Raas ya Korea inaelekea katika vita vikali vya kinuklea"-imesema kamati ya Korea ya kaskazini inayoshughulikia masuala ya amani katika eneo la Asia na Pacific,katika taarifa yake iliyochapishwa na shirika rasmi la habari la KCNA.Pindi vita vikiripuka hatutaki kuwaona wageni wanaoishi Korea ya kusini wakiingia hatarini."taarifa ya kamati hiyo imesema na kushadidia propaganda za utawala wa kikoministi unaoyasihi mashirika yote ya kigeni,makampuni na watalii wabuni mipango ya kuwahamisha wawakilishi wao.
Pyongyang iliyotega hivi karibuni makombora mawili ya masafa ya wastani katika mwambao wake wa mashariki,ilisema ijumaa iliyopita "haidhamini usalama wa wakala wowote wa kidiplomasia mjini Pyongyang kuanzia April kumi,ikiashiria uwezekano wa kufyetua kombora au kufanya jaribio la kinuklea.Hakuna nchi yoyote yenye uwakala wa kidiplomasia mjini Pyongyang iliyotilia maanani onyo hilo hadi sasa wanakiliangalia kama porojo tupu.
Viongozi wa Pyongyang wametekeleza lakini onyo la kuwarejesha nyumbani raia wake 53 elfu waliokuwa wakifanyakazi katika eneo la kiviwanda la nchi mbili za Korea-Kaesong lililoko katika ardhi yake.
Korea ya kusini yaelezea masikitiko yake
Korea ya kaskazini imewafungia njia tangu watumishi wa Korea ya kusini mpaka malori ya bidhaa kuingia katika eneo hilo lililokuwa likisifiwa kama mfano wa maana wa kojongeleana Korea mbili.
Rais wa Korea ya kusini Park Geun-Hye amesema "amevunjwa moyo na uamuzi wa Korea ya kaskazini wa kuwazuwia kwenda kazini raia wake katika eneo la Kaesong na wizara inayoshughulikia muungano imeahidi kudhamini usalama wa raia na kulinda milki yake.Serikali ya mjini Washington pia imeelezea masikitiko yake.
"Uamuzi huo hautaisaidia Korea ya kaskazini kulifikia lengo lake la kuimarisgha uchumi na hali ya maisha ya wakaazi wake" taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema.
China yatoa wito wa utulivu
Wakati huo huo Japan imesema hii leo imetega makombora chapa Patriot katika eneo la kati la mji mkuu Tokyo na mitambo ya kinga dhidi ya makombora itawekwa pia katika kisiwa cha Okinawa.Jeshi limepewa amri ya kuzuwia kombora lolote litakalolengwa dhidi ya nchi hiyo.Na jamhuri ya umma wa China,mshirika mkubwa wa Korea ya kaskazini imesema haitaki kuiona Raas ya Korea ikizamana katika bahari ya mtafaruku.Viongozi wa Beijing wanapinga hatua zozote zilizolengwa kuzidi kuhatarisha hali ya mambo-amesema hayo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Hong Lei wakati wa mazungumzo na waandishi habari hivi punde mjini Beijing.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo