Korea kusini yatarajia mateka waliosalia Afghanistan kuachiwa leo.
30 Agosti 2007Baadhi ya magazeti nchini Korea kusini yamepongeza makubaliano yaliofikiwa na Watalibani kuwaachia huru wakorea hao wafanyakazi wa jumuiya moja ya misaada ya kikiristo tarehe 19 mwezi uliopita, yakisema uamuzi wa serikali kuzungumza na watalibani ni mafanikio makubwa ya kidiplomasia.
Sambamba na hayo wakati serikali ikisema inatarajia mateka saba waliosalia kuachiwa huru leo, magazeti yameungana katika kulikosoa kanisa, na kusema serikali ilikua haina chaguo jengine bali kuzungumza na wateka nyara ili kuokoa maisha ya raia wake.
Watalibani waliwateka nyara jumla ya wakorea kusini 23 ambapo wawili kati yao waliuwawa hapo mapema,wawili wakaachiwa baadae na Jana wkawaachia 12 wengine kati ya 19 waliosalia.
Kiongozi mmoja wa kanisa la Presbyterian Kwon Kyuk-Soo alisema kutokana na dai la wizara ya mambo ya nchi za nje kwa familia za wahanga, sasa kanisa hilo ndilo litakalolipa tiketi za ndege kuwarudisha nyumbani mateka pamoja na gharama za kuisafirisha miili ya wenzao wawili waliouwawa.
Afisa huyo alisema kanisa litasitisha harakati zote za kidini na usambazaji misaada katika maeneo yote ya hatari na kwamba amearifiwa watumishi wa kujitolea waliotumwa na wengine pia wataondolewa ifikapo kesho.
Watalibani walitangaza wamekubali kuwaachia mateka waliosalia baada ya Korea kusini kuahidi itawaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan kama ilivyopangwa na kupiga marufuku wamisionari kwenda huko.
Marekani ilioikaribisha hatua hiyo ya kuachiwa huru mateka , ilikataa kutamka akama makubaliano ya kuachiwa kwa huru ni mfano mzuri au ni jambo la hatari. Kumekuweko na maoni tafauti juu ya uamuzi wa serikali ya Korea kusini kuzungumza moja kwa moja na waislamu hao wa msimamo mkali.
Wakati mateka saba waliosalia wakisubiriwa kuachiwa ili kuumaliza mkasa huo, hali ya usalama inaendelea kuwa mabaya. Mwanajeshi wa shirika la kujihami la magharibi NATO na mkalimani mmoja wa kiafgahan waliuawa leo wakati wa upigaji doria kusini mwa Afghanistan wanajeshi wengine wawili walijeruhiwa .
Kikitoa taarifa hiyo kikosi cha kimataifa cha NATO , hakikutaja uraia wa mwanajeshi aliyeuwawa au mahala pa tukio hilo, lakini wanajeshi walioko eneo la kusini hasa ni kutoka Uingereza, Canada ,Uholanzi na Marekani. Tukio hilo limeongeza idadi ya wanajeshi wa kimataifa waliouwawa Afghanistan mwaka huu kufikia 155.