1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kusini yadai Korea Kaskazini inapeleka askari Urusi

21 Oktoba 2024

Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini imewasilisha kwa balozi wa Urusi mjini Seoul malalamiko ya kupinga kile ilichokiita kupelekwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/4m24t
Askari wa Korea Kaskazini
Askari wa Korea KaskaziniPicha: Ahn Young-joon/AP/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini imewasilisha kwa balozi wa Urusi mjini Seoul malalamiko ya kupinga kile ilichokiita kupelekwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Urusi kwa ajili ya kupigana nchini Ukraine.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini, Kim Hong-kyunc, amesema ushiriki wa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita vya Ukraine utakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa na amesema hatua hiyo inatishia usalama wa Korea Kusini na kwingineko.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameishutumu Pyongyang kwa kujiandaa kuwapeleka wanajeshi 10,000 nchini Urusi, na ametoa wito wa kuijibu vikali hatua hiyo ya Korea Kaskazini.Korea Kaskazini yasema Korea Kusini ni kama taifa la "uadui"

Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, na mkuu wa Jumuiya ya NATO, Mark Rutte,  wamesema hakuna ushahidi wa uwepo wa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita vya nchini Ukraine. 

Urusi na Korea Kaskazini zimekanusha madai hayo lakini zimesema zimeimarisha uhusiano wa kijeshi, na kuzilitia saini mkataba wa ulinzi wa pande zote katika mkutano wao wa kilele uliofanyika mwezi Juni.