Korea Kusini kuijibu Korea Kaskazini kwa makombora
24 Novemba 2010Korea Kusini imesema itaishambulia Korea Kaskazini kwa makombora, iwapo nchi hiyo itachukua hatua zaidi za kiuchokozi. Hatua hiyo inatokana na shambulio lililofanywa na Korea Kaskazini katika kisiwa cha Korea Kusini mapema jana.
Pande hizo mbili zilifyatuliana risasi kwa muda wa saa moja, ikiwa ni moja kati ya mashambulio mabaya kabisa kutokea baina ya nchi hizo mbili kwa karibu miaka 60 iliyopita. Kiasi wanajeshi wawili wa Korea Kusini waliuawa huku wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa. Rais wa Korea Kusini, Lee Myung-bak amesema shambulio hilo linahitaji kujibiwa kwa nguvu.
Shambulio hilo limeshutumiwa vikali na jumuiya ya kimataifa. Rais Barack Obama wa Marekani amekiita kitendo hicho kama cha ''uchochezi na kuchukiza'' na kwamba Marekani itasimama katika kumlinda mshirika wake huyo. Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amezitaka pande zote mbili kujizuia na mazoezi.