1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yawaachia waandishi wa habari wa Marekani

Charo Josephat5 Agosti 2009

Uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini huenda uchukue mkondo mpya

https://p.dw.com/p/J3qZ
Waandishi wa Marekani baada ya kuachiwa huruPicha: AP

Korea Kaskazini imesema leo kwamba imewasamehe waandishi wawili wa habari raia wa Marekani baada ya rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Il mjini Pyongyang hapo jana.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton ameondoka nchini Korea Kaskazini mapema leo akiwa ameandamana na Laura Ling na Euna Lee wakielekea Los Angeles katika jimbo la Carlifonia nchini Marekani, ambako watajumuika na familia zao. Ikulu ya Marekani mjini Washington imesisitiza kuwa ziara ya Bill Clinton nchini Korea Kaskazini ilikuwa ya kibinafsi, lakini utawala wa Korea Kaskazini mjini Pyongyang, umesema unaiona ziara hiyo kuwa rasmi zaidi kuliko ya kibinafsi.

Shirika la habari la Korea Kaskazini limeripoti kwamba rais Kim Jong Il na Bill Clinton walifanya mazungumzo ya kina kuhusu maswala ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi kati ya Marekani na Korea Kaskazini kwa uwazi na kufikia makubaliano kuhusu kuachiwa kwa waandishi wawili wa habari wa kimarekani. Waandishi hao wamekuwa wakizuiliwa nchini Korea Kaskazini tangu mwezi Machi mwaka huu baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 12 jela na kazi ngumu kwa kuingia nchini humo kinyume na sheria.

Marafiki na familia za Laura Ling na Euna Lee zimefurahishwa na taarifa za kuachiwa kwa waandishi hao. Taarifa ya pamoja ya familia hizo imemshukuru rais wa Marekani, Barack Obama, waziri wa mashauri ya kigeni, Bi Hillary Clinton na wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, kwa kazi nzuri.

Akizungumza baada ya waandishi hao kuachiwa, babake Laura Ling, Doug Ling amesema, "Bila shaka nimefurahi sana. Hii ni moja kati ya siku za furaha kubwa maishani mwangu. Nilijua kitu kizuri kingetokea na kimetokea. Ninafuraha na ninashukuru watu wote waliotuombea. Naishukuru wizara ya mambo ya ndani na serikali kwa kufanya kila waliloweza kuwaokoa."

Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Al Gore, ameelezea furaha yake kwa kuachiwa Laura Ling na Euna Lee, ambao ni wafanyakazi wa televesheni ya Current mjini San Francisco aliyoianzisha Al Gore pamoja na Joel Hyatt.

Naye waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Hillary Clinton amewaambia waandishi wa habari mjini Nairobi Kenya mapema leo kwamba amefurahishwa na kufarijika na hatua ya kuachiwa huru Laura Ling na Euna Lee. Ameahidi kueleza kilichompeleka mumewe Bill Clinton nchini Korea Kaskazini mara tu Laura na Euna watakapoungana na familia zao.

China imeipongeza Korea Kaskazini kwa kuwaachia huru waandishi hao wa habari. Katika taarifa yake wizara ya mambo ya kigeni ya China imesema swala lililokuwa na umuhimu mkubwa limepata suluhiso linalofaa.

Korea Kaskazini imesema imewaachia waandishi hao baada ya Bill Clinton kuomba radhi kwa kitendo kiovu cha waandishi hao dhidi ya nchi hiyo. Lakini afisa aliyeandamana na Clinton katika ziara yake mjini Pyongyang, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amekanusha madai hayo akisema Clinton hakuomba msamaha.

Bill Clinton mit Kim Jong Il in Seoul, Südkorea
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton (kulia)na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong IlPicha: AP

Utawala wa Marekani umesema haukuihadi Korea Kaskazini kutarajia kitu chochote kutoka nchi za magharibi kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, kwa kuwakabidhi waandishi wawili wa habari kwa rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Korea Kaskazini iliwasilisha ombi la kutaka Bill Clinton azuru Pyongyang na utawala wa rais Obama ukaridhia kwa masharti kwamba ikubali kwanza kuwaachia huru waandishi hao na kwamba swala la nyuklia lisifungamanishwe na mzozo wa waandishi wa habari.

Ndege anamosafiria Bill Clinton, pamoja na waandishi wa habari Laura Ling na Euna Lee, imetua katika uwanja wa ndege wa jeshi la Marekani ya Misawa katika kisiwa cha Honshu nchini Japan kuongeza mafuta. Ndege hiyo tayari imeondoka kisiwani humo na inatarajiwa kuwasili kesho mjini Los Angeles.

Mwandishi:Josephat Charo

Mhariri:Aboubakary Liongo