1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yatilia mashaka kushiriki kwa Japan kwenye mazungumzo ya pande sita

19 Machi 2007

Mazungumzo ya pande sita juu ya Korea Kaskazini yamenza tena hii leo baada ya Marekani na Korea kaskazini kuutatua mzozo unaohusu dolla milioni 25.

https://p.dw.com/p/CHHu

Lakini bado Korea kaskazini inashaka shaka juu ya kushiriki kwa Japan kwenye mazungumzo hayo.

Mlango wa Mazungumzo juu ya mpango wa kinuklia wa Korea kaskazini umefunguliwa hii leo Beijing China baada ya Marekani kukubali kuachilia dolla milioni 25 za Korea Kaskazini ambazo ilikuwa imezizuia kufuatia shauku za baadhi ya maafisa wa Marekani kwamba fedha hizo huenda zinatumiwa na Korea kaskazini katika njia zisizohalali kuufadhili mpango wake wa Kinuklia.

Nchi sita zinazoshirika kwenye mazungumzo hayo zilikubaliana mnamo mwezi wa Februari kuipa Korea kaskazini siku 60 au hadi mwezi April kukifunga kinu chake cha Nuklia cha Yongbyon kwa ahadi kwamba itapewa msaada wa nishati na usalama.

Mjumbe wa Marekani Christopher Hill amesema wataingia kwenye duru nyingine ambayo inalengo la kuangalia jinsi ya kuzuia kinu cha Yongbyon kisifanye kazi pamoja na kuitaka nchi hiyo itangaze kikamilifu shughuli zake za kinuklia ikiwa ni pamoja na nchi inazoshirikiana nazo kwenye mradi huo.

Kwa upande wake Japan imekaribisha ufumbuzi wa mvutano huo wa fedha kati ya Korea kaskazini na Marekani lakini imeonya kwamba kuna kizingiti kingine kilichobakia ambacho ni kutekwa nyara kwa raia wake miaka kadhaa iliyopita.

Serikali ya Tokyo imeapa kwamba haitotoa mchango wake katika kuisaidia Korea kaskazini kiuchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mazungumzo ya pande sita hadi pale Pyongyang itakapokuwa wazi na suala la kutekwa nyara kwa raia wa Japan.

Korea kaskazini imekiri kuwateka nyara wajapan 13 katika miaka ya sabini na themanini kwa lengo la kuwafunza majasusi wake. Iliwarudisha watu watano na familia zao na kusema kwamba mateka wengine waliosalia walikufa lakini Japan inashikilia kuwa bado wapo hai na kwamba idadi ya raia wake waliotekwa nyara ni wengi zaidi kuliko inavyodaiwa na Korea kaskazini.

Aidha Korea kaskazini imeelezea wasiwasi wake juu ya kushiriki kwa Japan kwenye mazungumzo hayo ya pande sita. Mjumbe wa Korea kaskazini Kim Kye Gwan amehoji juu ya kuendelea kushiriki kwa Japan katika kikao hicho kilichoanza leo.

Wakati huo huo imearifiwa kuwa kinu cha Korea kaskazini cha Yongbyon cha kutengeneza mabomu ya atomiki kinaendelea kufanya kazi licha ya kwamba nchi hiyo iliahidi kukifunga. Mjumbe wa Korea kaskazini Kim Kye Gwan amesema hii leo nchi yake itakifunga kinu hicho pale vikwazo dhidi ya nchi yake vitakapoondolewa.

Mazungumzo yalioyanza leo ambapo Korea zote mbili kusini na kaskazini,China,Marekani Japan na Urussi zinashiriki yanatarajiwa kuchukua siku mbili.ingawa kuna kibarua kigumu kwani kabla ya kuanza mazungumzo ya leo Pyongyang ililaani ushirikiano wa kijeshi kati ya Korea kusini na Marekani uliopangiwa kuanza mwezi huu.Korea kaskazini imesema hatua hiyo inalenga kuharibu mazungumzo hayo.

Pia gazeti linalomilikiwa na serikali ya Korea kaskazini Rodong Sinmun limeasema Korea kaskazini iko tayari kwa yote mawili mazungumzo na Vita.