1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yatangaza mkakati wa kuishambulia Marekani

10 Agosti 2017

Korea Kaskazini limetangaza mkakati wake wa kurusha makombora mengine ambayo yataangukia kwenye kisiwa cha Guam kinachomilikiwa na Marekani siku moja baada ya Rais Donald Trump kuapa kuishambulia.

https://p.dw.com/p/2hz4v
Nordkorea Armee
Picha: picture-alliance/dpa/Kcna

Korea Kaskazini imetangaza hivi leo mpango wake wa kurusha kombora kuelekea kisiwa cha Guam, kituo kikuu cha kijeshi cha Marekani katika Bahari ya Pasifiki na kwahala ambako Marekani imeweka ndege zake za mashambulizi. 

Televisheni ya taifa ya Korea Kaskazini imemuonesha mkuu wa mikakati jeshini, Kamanda Kim Rak Gyom, huku mtangazaji akisoma tamko la kamanda huyo linalochambua undani wa namna kombora hilo litakavyorushwa.

"Makombora ya Hwasong-12 yatakayorushwa na Jeshi la Watu wa Korea yatavuuka anga la Shimane, Hiroshima na Koichi nchini Japan, yakiruka umbali wa kilomita 3,356.7 kwa sekunde 1,065 kabla ya kutua kwenye bahari iliyo umbali wa kati ya kilomita 30 hadi 40 kutoka kisiwa cha Guam", inasema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kamanda Kim Rak Gyom, maroketi hayo yanapangwa kurushwa kabla ya mwishoni mwa wiki ijayo. Kisiwa hicho kidogo kina wanajeshi 7,000 wa Marekani kwenye vituo vyake viwili, na kinakaliwa na wakaazi 160,000. 

Ni jambo la nadra sana kwa Korea Kaskazini kutangaza undani wa urushaji wake wa makombora kama hivi ilivyofanya leo (Agosti 10), lakini endapo kweli itachukuwa hatua hiyo, hicho kitakuwa kitendo kikubwa cha uchokozi kuwahi kufanywa na nchi hiyo ndani ya kipindi chote cha mzozo wake na Marekani.

Vita vyanukia?

Korea Kusini, Korea Kaskazini, Marekani
Mwanajeshi wa Korea Kusini akipita kando ya kioo cha televisheni kinachoonesha masafa kati ya Korea Kaskazini na kisiwa cha Guam katika kituo cha treni mjini Seoul tarehe 9 Agosti 2017.Picha: Getty Images/AFP/J. Yeon-Je

Tamko hili la sasa linaashiria kilele cha mzozo wa maneno baina ya Pyongyang na Washington, baada ya hapo jana Rais Donald Trump kuionya Korea Kaskazini kwamba ingekabiliana na "moto na ghadhabu" ikiwa ingeliitisha Marekani.

"Kiongozi wa Korea Kaskazini amekuwa akitishia sana, zaidi ya hata kauli za kawaida na kama nilivyosema, Korea Kaskazini itakumbana na moto, ghadhabu na nguvu za kweli, ambazo kamwe hazijawahi kushuhudiwa duniani hapo kabla."

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini, KCNA, limeileleza kauli hiyo ya Trump kuwa ni kitisho kilichojaa upuuzi, na kwamba jeshi la nchi hiyo linapanga "kuvishambulia vikosi vya adui kwenye vituo vyake kisiwani Guam na kutuma onyo muhimu kwa Marekani".

Kwa upande mwengine, Korea Kusini imeitolea wito Korea Kaskazini kuacha kufanya mambo ambayo yataleta balaa kwenye Rasi ya Korea. Msemaji wa Ikulu ya Blue House, Park Su-hyun, amesema kuwa serikali itasaka njia za kuutatua mzozo huo kwa kushirikiana na nchi nyengine.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga