1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa umeshapinga majaribio hayo ya makombora

Admin.WagnerD7 Desemba 2017

Vuta  nikuvute baina ya nchi mbili zenye mabavu, Marekani na Korea Kaskazini , inatajwa kuchochea  kuzuka kwa vita.  Ingawa haijulikani ni lini vita hiyo itaibuka lakini hofu kubwa imeendelea kutanda.

https://p.dw.com/p/2ox0b
Kim Jong Un, Donald Trump
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Marekani, Donald Trump.Picha: picture alliance/AP Photo

 Vita haviwezi kuepukika. Hivyo ndivyo wanavyosema  Korea ya Kaskazini. Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amesema  mafunzo makubwa ya kijeshi yanayofanywa na Marekani na Korea Kusini, pamoja na vitisho vya Marekani vya kuanza vita dhidi ya Pyongyang, vimesababisha uwezekano wa kuzuka kwa vita katika rasi ya Korea kuwa jambo la uhakika.

 Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje wa Korea Kaskazini, alilaani maneno ya kuchochea vita yanayotolewa na maofisa wa Marekani ambayo yanachochea rasi hiyo kuingia katika vita.

 Swali lililobaki sasa ni lini vita vitaanza? Msemaji wa Wizara ya nje ya Korea Kaskazini alisema jana jioni katika tamko lake lililotolewa na kituo rasmi cha habari cha Korea Kaskazini cha KCNA

``Hatuombei vita, lakini hatuwezi kujificha.`` amesema Msemaji huyo

Kadhalika, Mtangazaji wa Kituo cha Habari cha Korea Kaskazini, cha KTR alitangaza akisema:

´`Mazoezi makubwa ya vita vya kinyuklia yanayofanywa na Marekani yanaendelea kuleta hali tete katika rasi ya Korea. Mfululizo wa kauli za kuchochea vita zinazotolewa na maofisa wa juu wa Marekani, katika hali kama hii, umesababisha kuibuka kwa vita katika rasi ya Korea na sasa vita  inaaminika kuwa jambo la uhakika,``

Hofu katika rasi ya Korea, imeongezeka katika miezi ya karibuni baada ya Korea ya Kaskazini kufanya majaribio ya hivi karibuni ya makombora ya kinyuklia.

Korea Kaskazini inafanya hayo yote wakati kukiwa na shinikizo la kupingwa la  kimataifa na maazimio yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa.

Nordkorea Raketentest in Pjöngjang
Moja ya makombora yaliyofanyiwa majaribio na Korea Kaskazini. Picha: Getty Images/AFP/STR

Korea Kaskazini wiki iliyopita ilifanya majaribio ya makombora ya kimaabara ya kisasa zaidi  ambayo yanauwezo  uwezo wa kufika Marekani.

 Mshauri Marekani aonya kuzuka kwa vita

Mshauri wa  masuala ya ulinzi wa Ikulu ya Marekani, H. R MacMaster amesema mwishoni mwa wiki hii kuwa, uwezekano wa vita na Korea kaskazini unaongezeka kila siku.

 Seneta wa Republican  Lindsey Graham ameitaka  Wizara ya Ulinzi ya Marekani, kuanza kuwaondoa  Korea Kusini, wanafamilia wa wanajeshi ikiwamo wenza na watoto. Amesema  mgogoro wa Korea Kaskazini unaongezeka.

Wasiwasi wa kuzuka kwa vita umeongezeka zaidi baada ya ziara isiyo ya kawaida  katika nchi hiyo iliyotengwa kimataifa, iliyofanywa na Mkuu wa masuala ya siasa wa Umoja wa mataifa Jeffrey Feltman mapema wiki hii.

Ni ziara rasmi na ya kiwango cha juu  kuwahi kufanywa na ofisa wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2012 katika eneo hilo la Korea Kaskazini.

Shirika la  habari la Korea Kaskazini, KCNA limebainisha kuwa, Naibu Waziri wa mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Pak Myong alikutana na Feltman jana na wakajadilia masuala ya ushirikiano na masuala mengine.

Hata hivyo katika hotuba yake ya mwezi Septemba katika Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  Waziri wa Mambo ya nje wa Korea Kaskazini, Ri, aliitetea nchi yake akisema, majaribio ya makombora ya kinyuklia, ni mipango ya kujilinda dhidi ya Marekani na vitisho vya nyuklia.

 Mwandishi: Florence Majani(AP; Reuters)

Mhariri: Yusuf Saumu